WASIRA; KUFANYA ZIARA YA KIKAZI KILIMANJARO, KUKAGUA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM

MOSHI-KILIMANJARO.


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, anatarajiwa kuwasili mkoani Kilimanjaro Juni 4, 2026 kwa ajili ya ziara ya kikazi ya chama, ambapo atatembelea maeneo mbalimbali na kufanya mikutano ya ndani na viongozi wa CCM katika ngazi tofauti za uongozi.

Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake, Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Abraham Urio, alisema maandalizi ya ziara hiyo yamekamilika na uongozi wa chama mkoani humo uko tayari kumpokea kiongozi huyo.

Alisema Wasira atawasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Juni 4, ambapo atapokewa na viongozi wa CCM wa mkoa huo kabla ya kuanza rasmi shughuli za ziara yake.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, Juni 5 Wasira atatembelea ofisi za CCM Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo atapokea taarifa mbalimbali za utekelezaji wa shughuli za chama kabla ya kufanya kikao cha ndani na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa.

Urio alisema Juni 6, Makamu Mwenyekiti huyo atakuwa Wilaya ya Rombo ambako atafanya kikao cha ndani na mabalozi wa mashina, viongozi wa mabaraza ya jumuiya mbalimbali za chama pamoja na wazee mashuhuri wa CCM.

Aidha, Juni 7, atakuwa Manispaa ya Moshi ambapo atafanya kikao cha ndani kitakachofanyika katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, katika kikao hicho atakutana na wazee wa chama, viongozi wa mabaraza ya jumuiya zote za CCM pamoja na viongozi wa mashina, maarufu kama mabalozi.

Aliongeza kuwa Juni 8 Wasira atatembelea Wilaya ya Same, ambapo atashiriki shughuli za kijamii kabla ya kufanya kikao cha ndani na viongozi wa mashina, viongozi wa jumuiya za chama, mabaraza mbalimbali na wazee wa chama, baadaye atahutubia mkutano wa hadhara utakaofanyika katika viwanja vya CCM Wilaya ya Same

Alisema ziara za viongozi wa CCM zina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya chama na Taifa, kwani zinatoa fursa ya kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM ambayo ni msingi wa ahadi zilizotolewa kwa wananchi wakati wa uchaguzi.

“Wakati wa Uchaguzi Mkuu tuliinadi Ilani ya CCM na kuwaeleza wananchi mambo mbalimbali ambayo chama na Serikali vitayatekeleza, hivyo ni muhimu kwa CCM kufuatilia na kukagua yale iliyoahidi wananchi ili kuhakikisha yanatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi,” alisema Urio.

Aliongeza kuwa l ziara hiyo pia itatoa nafasi kwa viongozi wa chama kusikiliza maoni ya wanachama na wananchi kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na kuimarisha mshikamano ndani ya CCM.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.