MOSHI-KILIMANJARO.
WADAU wa maendeleo mkoani Kilimanjaro wamepongeza mpango wa kuanzishwa kwa Maktaba ya Mkoa na Makumbusho Jumuishi ya Kilimanjaro, wakisema hatua hiyo itasaidia kuhifadhi historia, utamaduni na mali kale za Watanzania, ikiwemo urithi uliobebwa na kupelekwa nje ya nchi wakati wa ukoloni wa Kijerumani.
Maoni hayo yalitolewa Juni Mosi, 2026, wakati wa kikao cha uwasilishaji wa mpango wa kuanzishwa na kusanifiwa kwa Makumbusho Jumuishi ya Kilimanjaro, kilichofanyika katika ukumbi wa KDC wilayani Moshi na kuwashirikisha viongozi wa serikali, wataalamu wa utamaduni, viongozi wa kimila na wadau wa sekta ya utalii.
Wakichangia mada mbalimbali katika kikao hicho, Afisa Utamaduni wa Wilaya ya Hai, Stanley Evance, pamoja na maafisa utamaduni Albetha Makule, Peter Tungu na mdau kutoka sekta binafsi Bosco Simba, waliupongeza mpango huo wakisema utatoa fursa kwa watafiti, wanafunzi na wadau wa utamaduni kupata maarifa kuhusu historia, sayansi ya utamaduni na uhifadhi wa mali kale.
Walisema uwepo wa maktaba na makumbusho hayo utaifanya Kilimanjaro kuwa kituo muhimu cha tafiti za kihistoria na kitamaduni, huku ukichangia kuhamasisha kizazi cha sasa na kijacho kutambua na kuthamini urithi wa taifa.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Mkurugenzi wa Kanda ya Kaskazini wa Makumbusho ya Taifa, Agnes Robert, aliupongeza uongozi wa halmashaurinya Moshi kwa kuanzisha wazo hilo, akieleza kuwa litakuwa na mchango mkubwa katika kuhifadhi historia ya Tanzania kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Wilayaya Moshi Beno Chuwa, alisema kuweko kwa makumbusho hiyo mkoani Kilimanjaro, wanafunzi kutoka vyuo vikuu nchini, watakuja kujifunza mchango wa Mangi Rindi Mandara, jinsi alivyokuwa mwana diplomasia hapa nchini.
Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Mratibu wa Makumbusho ya MDC, Dk. Venance Silayo, alisema tayari jengo hilo ambalo lilikuwa likitumiwa na machifu wameshalifanyia ukarabati ili kuweza kufungua makumbusho ya mkoa wa Kilimanjaro.
Aidha Dk. Silayo ambaye pia ni Mhadhiri wa Akiolojia na Turathi, Idara ya Akiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema takwimu zinaonesha kuwa kuna mabaki zaidi ya 100,000 yanayohusiana na Watanzania yaliyopo nchini Ujerumani, zaidi ya 2,000 nchini Hungaria na mengine mengi katika nchi mbalimbali ikiwemo Uingereza na Ufaransa.
Akifungua mkutano wa wadau wa maendeleo uliolenga kujadili na kushauriana kuhusu uanzishwaji wa makumbusho hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Shadrack Mhagama;
Alisema kuwa mwaka 2023, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliunda kamati maalum ya kuratibu urejeshaji wa mabaki hayo kufuatia makubaliano yaliyofikiwa kati yake na Frank-Walter Steinmeier wakati wa ziara yake nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Mhagama, alisema mpango wa kurejesha mabaki hayo unalenga pia kurudisha maelfu ya vitu vya kihistoria na kitamaduni vilivyoondolewa nchini wakati wa ukoloni na kupelekwa katika makumbusho mbalimbali duniani.
Kikao hicho kiliwakutanisha Wakurugenzi wa halmashauri zote za Mkoa wa Kilimanjaro, maafisa utamaduni, viongozi wa kimila, wataalamu wa sekta ya utalii pamoja na wadau wengine wa maendeleo kwa lengo la kujadili namna bora ya kuanzisha na kuendeleza maktaba na makumbusho yatakayohifadhi historia na urithi wa taifa.














