MOSHI-KILIMANJARO.
UMOJA wa Machifu Mkoa wa Kilimanjaro umesema utaendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anazozifanya katika kuwaletea maendeleo Watanzania, huku ukiahidi kusimama naye na kulinda mafanikio ya taifa kwa nguvu zote.
Kauli hiyo ilitolewa Mei 30,2026 na Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Mkoa wa Kilimanjaro, Chifu Frank Marialle, wakati wa hafla ya kumkabidhi ngao na mkuki Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Stendi Ndogo ya Mabasi mjini Moshi.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa mila na desturi wa mkoa huo, wakiwemo machifu, wafumwa na malaigwanani, Chifu Marialle alimkaribisha Kihongosi mkoani Kilimanjaro na kumpongeza kwa mchango wake katika kuimarisha mshikamano na maendeleo ya taifa.
“Kwa niaba ya viongozi wa mila na desturi wa Mkoa wa Kilimanjaro, ninakukaribisha sana katika mkoa wetu. Leo tunakupatia mkuki na ngao kama ishara ya heshima, ukaribisho, uongozi na mamlaka katika jamii zetu,” alisema.
Alifafanua kuwa vifaa hivyo vya jadi vinaashiria ulinzi, busara, ujasiri na wajibu wa kuwatumikia wananchi kwa uadilifu, uzalendo na kujitolea kwa maslahi ya taifa.
Chifu Marialle alimtaka Kihongosi kuendelea kumsaidia na kusimama imara pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan katika kukabiliana na changamoto mbalimbali na wale wanaopinga juhudi za maendeleo ya taifa.
“Tunakuomba uendelee kumsaidia, kumlinda na kusimama imara pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan dhidi ya changamoto na maadui wa maendeleo ya taifa letu,” alisema.
Aidha, aliwashukuru viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kilimanjaro kwa ushirikiano wao katika kuwaletea wananchi maendeleo, akiwataja Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, pamoja na wabunge wa mkoa huo.
Alisema umoja wa viongozi wa mila, Serikali na CCM umekuwa nguzo muhimu katika kudumisha amani, mshikamano na maendeleo ya wananchi wa Kilimanjaro.
![]() |









