KIHONGOSI: MSIWAKABIDHI WATU WASIO NA LESENI YA KUONGOZA NCHI

MOSHI-KILIMANJARO.


KATIBU wa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amewataka wananchi kuendelea kukiamini CCM kwa kuwa kina uzoefu na uwezo wa kuongoza taifa na kusimamia maendeleo ya wananchi.

Kauli hiyo ameitoa Mei 30,2026, wakati akizindua Shina Namba Mbili katika Kata ya Njoro, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ambapo amewataka wananchi kutowakabidhi madaraka watu wasiokuwa na uwezo wa kuongoza nchi.

Alisema ujenzi wa taifa ni mchakato wa muda mrefu unaohitaji mipango, rasilimali na utekelezaji wa hatua kwa hatua, akibainisha kuwa serikali imekuwa ikiendelea kuboresha huduma za kijamii kila inapopata fedha kwa kujenga barabara, vituo vya afya, vyumba vya madarasa pamoja na kupeleka miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini.



Aliwataka Wananchi wasidanganywe na wanasiasa wanaodai kwamba wakipewa dhamana leo, kesho watatatua changamoto zote za maji, umeme na barabara, kujenga nchi si jambo la siku moja, ni mchakato unaohitaji muda na ushirikiano wa wananchi na serikali.

Aidha, alikosoa baadhi ya vyama vya siasa kwa madai ya kuhamasisha maandamano na vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na mshikamano wa taifa, akisisitiza kuwa madhara ya vurugu hizo mara nyingi huwakumba wananchi wa kawaida badala ya viongozi wanaohamasisha shughuli hizo.

Alisema wananchi wanapaswa kulinda umoja na mshikamano uliodumu kwa miaka mingi nchini, huku wakikataa ushawishi wowote unaoweza kuhatarisha amani na utulivu wa taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shina namba mbili, tawi la Bohora, Kata ya Njoro, Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro

Maziora Msuya, amewasisitizia Wanachama wa CCM na jumuiya zake kuendelea kulipa ada za uanachama na kwamba uimara wa CCM unaanzia ngazi ya shina kupitia ushiriki na mchango wa wanachama wake.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.