KIHONGOSI; AWAPONGEZA WATAALAM WA HOSPITALI YA KIBONG’OTO KWA UTOAJI WA HUDUMA BORA

SIHA-KILIMANJARO.


KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, amewapongeza Wataalam wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH) kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kutoa huduma za afya kwa wananchi.

Kihongosi alitoa pongezi hizo Mei 29,2026, Wilayani Siha, wakati alipotembelea hospitali hiyo kwa lengo la kujionea utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa hospitalini hapo, ambapo alieleza kuridhishwa na matumizi ya fedha pamoja na ubora wa miradi inayoendelea.

Alisema kazi ya kuwahudumia wagonjwa ni ngumu na inahitaji moyo wa kujitolea, huruma na upendo mkubwa kwa binadamu, akibainisha kuwa si kila mtu anaweza kufanya kazi ya taaluma ya afya kutokana na changamoto zake.

Aidha, alisema hospitali hiyo ina historia kubwa nchini kwani ilianzishwa mwaka 1926, na ifikapo Oktoba mwaka huu itatimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwake.

Mafundi ujenzi wakiendelea  na ujenzi katika Jengo la Utawala Kibong’ota 

Alisema Serikali imeendelea kuiboresha hospitali hiyo kwa kujenga miundombinu mipya kadri fedha zinavyopatikana, ambapo tangu mwaka 2023 hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 38 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katibu huyo wa NEC, amewataka wananchi wa Wilaya ya Siha kuhakikisha wanailinda na kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, alimpongeza Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Leonard Subi, pamoja na timu yake kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa hospitalini hapo.

Pia aliipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Kamati ya Usalama ya Mkoa kwa namna wanavyosimamia fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Kwa upande Meneja wa Maabara ya Afya ya Jamii Daraja la Tatu Kibong’oto (KIDH), Dk. Shaban Mziray, alisema maabara hiyo, ikianza kutumika mwaka 2023 na imekuwa na mchango katika ufuatiliaji wa magonjwa ya milipuko, pamoja na tafiti mbalimbali za afya.

Dk. Mziray alisema miongoni mwa kazi ambazo zinafanyika katika maabara hiyo ni pamoja na kufuatilia usugu wa vimelea dhidi ya dawa, kubaini magonjwa ya kuambukiza katika jamii, yakiwemo kifua kikuu cha kawaida, kifua kikuu sugu pamoja na kufa ya tafiti za kimkakati za kuboresha tiba.

Ziara ya Katibu Itikadi, Uenezi na Mafunzo mkoani Kilimanjaro imelenga kukagua Uhai wa Chama, kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.