MOSHI-KILIMANJARO.
DIWANI wa Kata ya Bomambuzi, Juma Raibu Juma, amechinja mbuzi 105 kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Eid Al-Adha na kugawa nyama kwa wananchi mbalimbali, wakiwemo wenye mahitaji maalum.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, diwani huyo alisema hatua hiyo imelenga kushirikiana na waumini wengine wa dini ya Kiislamu katika kuadhimisha sikukuu hiyo muhimu kwa vitendo vya upendo, mshikamano na kusaidia jamii yenye uhitaji.
Alisema nyama hiyo imegawiwa katika vituo vya watoto yatima, vituo vya kulelea wazee, familia zisizojiweza pamoja na wananchi wengine wa kawaida ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki furaha ya Eid Al-Adha.
Aidha, ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kujenga tabia ya kupendana, kusaidiana na kudumisha mshikamano katika jamii, akieleza kuwa kufanya hivyo kutaiwezesha nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu.
“Ni muhimu kutumia sherehe mbalimbali kuonyesha upendo kwa wengine, hasa wenye mahitaji, kwani hali hiyo huimarisha mshikamano na umoja miongoni mwa wananchi,” alisema.
Kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu, ibada ya kuchinja mnyama katika Sikukuu ya Eid Al-Adha inatokana na simulizi ya Nabii Ibrahim aliyemtii Mwenyezi Mungu baada ya kuota akiamrishwa kumchinja mwanawe kama mtihani wa imani na utiifu wake.





