CHAMI AWASHUKURU TANAPA, AZANIA BANK KWA KUKUZA UTALII JUMUISHI KWA WENYE ULEMAVU

MOSHI-KILIMANJARO.

MKURUGENZI wa Kilimanjaro Disability Royal Tour and Safaris, Deogratius Chami, amelishukuru Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na Azania Bank, kumwezesha kupanda Mlima Kilimanjaro na kufika kilele cha Uhuru Peak mara mbili, akisema hatua hiyo ni ushahidi kuwa watu wenye ulemavu wanaweza kushiriki kikamilifu katika sekta ya utalii wakipewa fursa na ushirikiano unaostahili.

Chami, ambaye ni Mtanzania wa kwanza mwenye ulemavu wa viungo kupanda Mlima Kilimanjaro kwa kutumia kiti mwendo hadi kilele cha Uhuru Peak chenye urefu wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari, alisema mafanikio hayo yasingewezekana bila msaada wa wadau mbalimbali waliomuamini na kumwezesha kutimiza ndoto yake.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi baada ya kushiriki mbio za Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Chami aliwataka wafadhili, taasisi za umma na binafsi kuendelea kuwawezesha watu wengine wenye ulemavu ili nao wapate nafasi ya kuonyesha uwezo wao.

"Naishukuru TANAPA na Azania Bank kwa kuniamini na kuniwezesha kupanda Mlima Kilimanjaro, nawaomba wasiishie kwangu pekee, waendelee kuwasaidia watu wengine wenye ulemavu kwa sababu wana mchango mkubwa kwa taifa na jamii," alisema.

Pia alimshukuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Mwajuma Nasombe, kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika mbio za Mwenge wa Uhuru, akisema ushiriki huo umeendelea kuhamasisha jamii kutambua uwezo wao na kuendeleza kampeni ya utalii jumuishi yenye kaulimbiu ya "Utalii Jumuishi Unaanza na Sisi."

Chami alisema; utalii jumuishi unapaswa kuanzia Tanzania na kuenea duniani kote, huku akisisitiza kuwa watu wenye ulemavu si walengwa wa misaada pekee bali ni wadau muhimu wanaoweza kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya utalii.

Kwa mujibu wa Chami, alisema jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kutetea haki za watu wenye ulemavu zimeongeza utambuzi wao katika jamii na kufungua fursa nyingi zaidi za ushiriki katika shughuli za maendeleo.

Alisema kuanzishwa kwa kampeni ya Royal Tour kumetoa mchango mkubwa katika kuitangaza Tanzania kimataifa, jambo ambalo limemhamasisha kuunga mkono juhudi hizo kupitia dhana ya Utalii Jumuishi.

"Nilipopewa nafasi nilithibitisha kuwa kupanda Mlima Kilimanjaro kunawezekana hata kwa mtu mwenye ulemavu, nimeufikia mara mbili, hivyo ninawahamasisha watu wengine wenye ulemavu kutoka Tanzania na duniani kote kuja kupanda mlima huu mrefu zaidi barani Afrika," alisema.

Chami alieleza kuwa Utalii Jumuishi una manufaa makubwa kiuchumi, akibainisha kuwa mtalii mwenye ulemavu kutoka nje ya nchi mara nyingi husafiri akiwa na wasaidizi, ndugu au wataalamu zaidi ya 10, hali inayoongeza idadi ya wageni wanaotumia huduma mbalimbali za utalii na hivyo kuongeza mapato ya fedha za kigeni nchini.

"Si kweli kwamba watu wenye ulemavu hawawezi kuliingizia taifa mapato. Mtalii mwenye ulemavu anapokuja nchini huambatana na watu wengi zaidi wanaotumia huduma za malazi, usafiri, chakula na vivutio vya utalii, huo ni mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa," alisema.

Aidha Chami alitoa wito kwa Serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kuendelea kuwainua watu wenye ulemavu kwa kuwawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, akisema uwekezaji kwao ni uwekezaji wenye tija kwa taifa.

"Nilipewa nafasi nikafika hapa nilipo leo. Wapo watu wengi wenye uwezo kama wangu wanaosubiri kuaminiwa na kupewa fursa, tukiwainua, nao wataisaidia Tanzania kupitia Utalii Jumuishi na sekta nyingine za maendeleo," alisema.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.