MOSHI-KILIMANJARO.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Moshi imesema haijabadilisha matumizi ya eneo lolote la wazi, ikieleza kuwa kinachoendelea katika eneo la Uhuru Park ni utekelezaji wa mpango wa muda mrefu wa kuboresha eneo hilo bila kuathiri matumizi yake ya awali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Francis Shio, amesema eneo la Uhuru Park lina hati miliki ya halmashauri na tangu awali lilipangwa kutumika kama eneo la wananchi kupumzika na kufanyia shughuli mbalimbali za kijamii.
Amesema ujenzi unaoendelea wa vibanda vinavyozunguka eneo hilo ni sehemu ya mpango wa kulijengea uzio, kuweka mageti ya kuingilia na kutokea pamoja na kuimarisha usalama na mazingira ya bustani hiyo.
"Mpango huu si wa leo. Miaka ya nyuma tayari halmashauri ilijenga vibanda takribani 39 katika eneo hilo. Sasa tunaendelea na hatua nyingine za utekelezaji wa mpango huo," alisema Shio.
Alieleza kuwa baada ya kukamilika kwa uzio, eneo hilo litaboreshwa kwa ndani kwa kuweka sehemu za watoto kuchezea, maeneo ya mapumziko na huduma nyingine zitakazowezesha wananchi kulitumia kwa usalama zaidi.
"Lengo letu si kubadilisha matumizi ya eneo hili, bali kulifanya liwe salama na lenye huduma bora. Mzazi atakapomleta mtoto wake atakuwa na uhakika wa usalama kutokana na uwepo wa uzio," alifafanua.
Shio alisema fedha zinazotumika kujenga uzio huo zinatokana na mapato ya ndani ya halmashauri, huku akibainisha kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, ukurasa wa 58, ibara ya 95, inaelekeza ujenzi wa maduka yanayozunguka eneo la Uhuru Park kwa lengo la kukuza shughuli za biashara na kuongeza mapato.
Akizungumzia eneo la Shanty Town, alisema nalo lina hati ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na matumizi yake yamepangwa kuwa ya biashara, ambapo tayari limetangazwa kupitia utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) kwa ajili ya kupata wawekezaji.
Alisema hatua hiyo inalenga kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri na kuharakisha maendeleo ya mji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, alisema ofisi yake haijabadilisha matumizi ya ardhi katika eneo lolote.
Alisema baada ya Waziri Mkuu kuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kufuatilia suala hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ilitembelea eneo husika na taarifa ya uchunguzi itawasilishwa serikalini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro amethibitisha kupokea maelekezo hayo kutoka kwa Waziri Mkuu na amesema Juni 29, mwaka huu, atazungumza na waandishi wa habari kuhusu suala hilo.
Hoja ya matumizi ya eneo la Uhuru Park iliibuliwa bungeni na Mbunge wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, aliyemtaka Serikali kutoa msimamo wake kuhusu viongozi wanaodaiwa kukiuka matumizi ya maeneo ya wazi, akidai kuwa eneo hilo limebadilishiwa matumizi.
![]() |












