KCMC YALETA NAFUU KWA WAGONJWA WA SARATANI KANDA YA KASKAZINI

MOSHI-KILIMANJARO 

WANANCHI wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini wanaougua saratani wanatarajiwa kunufaika kwa kiasi kikubwa na huduma ya tiba ya mionzi inayotolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya Chuo cha Tiba cha Kikristo Kilimanjaro (KCMC), hatua itakayopunguza safari ndefu na gharama za kufuata matibabu Jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa Juni 22,2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC Profesa Gileard Masenga, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya huduma hiyo hospitalini hapo.

Alisema asilimia 60 hadi 70 ya wagonjwa wenye changamoto ya saratani wanahitaji tiba ya mionzi, hivyo wananchi ambao wako ukanda wa Kaskazini watanufaika na huduma ya matiba u ya mionzi karibu na maeneo yao.

Profesa Masenga alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo kumeondoa adha kwa wagonjwa kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara ambao hapo awali walilazimika kusafiri zaidi ya kilometa 600 kwenda Dar es Salaam kupata matibabu ya mionzi.

Alisema tangu mwezi Februari mwaka huu huduma hiyo ilipoanza kutolewa, zaidi ya wagonjwa 80 tayari wamepata matibabu, huku hospitali ikipokea wastani wa wagonjwa zaidi ya 30 kwa siku wanaohitaji huduma za saratani.

“Matibabu ya mgonjwa mmoja yanaweza kuchukua takribani wiki sita, hivyo uwepo wa huduma hii hapa KCMC unawapunguzia wagonjwa gharama kubwa za usafiri, malazi na muda wa kukaa mbali na familia zao,” alisema.


Alibainisha kuwa ujenzi wa jengo la tiba ya mionzi pamoja na ununuzi wa vifaa tiba umegharimu jumla ya Sh bilioni 17, ambapo Serikali imechangia Sh bilioni 5.5 huku wadau mbalimbali wakichangia zaidi ya Sh bilioni 6 pamoja na vifaa tiba.

Profesa Masenga alisema jengo hilo lina uwezo wa kubeba mashine tano za tiba ya mionzi, lakini kwa sasa lina mashine mbili zinazowezesha kuhudumia wagonjwa 1,500 kwa mwaka, mashine zote tano zitakapowekwa uwezo huo utaongezeka na kufikia wagonjwa 5,000 kwa mwaka.

Alisema saratani ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza yanayoongoza kwa sasa nchini Tanzania, Afrika Mashariki na duniani kote, huku KCMC ikishuhudia ongezeko la wagonjwa wenye magonjwa hayo.

“Kati ya wagonjwa 10 wanaolazwa KCMC, wanane wanaugua magonjwa yasiyoambukiza pamoja na majeraha ya ajali, huku wawili pekee wakiwa na magonjwa ya kuambukiza,” alisema.

Aliongeza kuwa hospitali hiyo ina wataalamu wanane wa tiba ya saratani na wengine wanaendelea na masomo ya juu kupitia ufadhili mbalimbali, ikiwemo Mfuko wa Elimu wa Dk. Samia Suluhu Hassan, ili kuongeza uwezo wa kutoa huduma bora za matibabu ya saratani.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.