MBUNGE WA JIMBO LA MWANGA DK NGWARU JUMANNE MAGHEMBE AKABIDHI MIPIRA YA MAJI KITOGOTO

MWANGA-KILIMANJARO.

MBUNGE wa Jimbo la Mwanga, Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe, amekabidhi mipira ya kusambazia maji kwa Serikali ya Kijiji cha Kitogoto, kilichopo Kata ya Kivisini Wilayani Mwanga, ikiwa ni jitihada za kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa eneo hilo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Dkt. Maghembe alisema kijiji hicho kimekuwa kikikabiliwa na uhaba mkubwa wa maji hali iliyowalazimu wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo, jambo lililosababisha adha kubwa kwa familia nyingi.

Mbunge huyo alisema utoaji wa mipira hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni, akisisitiza kuwa ataendelea kushughulikia changamoto zote zinazowakabili wananchi wa Jimbo la Mwanga katika kipindi chote cha miaka mitano ya uongozi wake.

Mipira hiyo ilikabidhiwa kwa niaba ya mbunge na Katibu wake, Jeremiah Boniphace Mziray, ambaye alisema itarahisisha usambazaji wa maji katika kijiji hicho na kupunguza kero ya wananchi, huku akitoa wito kwa jamii kushirikiana kuitunza miundombinu hiyo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kitogoto, Rashid Ibrahim Mkizungo, alimshukuru mbunge kwa kutimiza ahadi hiyo akisema kwa muda mrefu wananchi walilazimika kutumia maji ya mito ambayo si salama kiafya kutokana na ukosefu wa huduma ya maji safi.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kivisini, Mwalimu Mziray, alisema mradi huo wa maji utanufaisha wananchi zaidi ya elfu nne wa kijiji hicho na maeneo ya jirani ambao awali walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata maji.

Nao wananchi wa Kitogoto, akiwemo Saidati Ramadhani Mnzava, Mwanafatuma Kadori na Bonny Mdee, walimshukuru mbunge kwa kuanza kutekeleza ahadi zake mapema, wakisema mipira hiyo itapunguza adha ya kutembea hadi kilometa tano kufuata maji na kuboresha ustawi wa familia zao.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.