MOSHI-KILIMANJARO.
MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai, ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuanzisha mafunzo ya wasaidizi wa huduma za anga katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kilimanjaro (Moshi RVTSC) ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi na ajira.
Swai alitoa ombi hilo Julai 7,2025 kwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, akisema Moshi ina uwanja wa ndege ambao ukikamilika unatarajiwa kupokea ndege nyingi, hivyo ni muhimu kuwaandaa vijana wa eneo hilo kufanya kazi katika sekta ya anga.
Alisema kuanzishwa kwa mafunzo hayo VETA Moshi kutasaidia vijana wengi kupata ajira na kupunguza utegemezi wa ajira kutoka nje ya mkoa, huku akiipongeza VETA Moshi kwa mchango wake katika kuwajengea vijana ujuzi wa ufundi stadi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, aliwaelekeza madiwani na wataalamu wa Manispaa ya Moshi kufanya ziara ya kutembelea chuo hicho ili kujionea programu zinazotolewa kabla ya kuzifanyia maamuzi katika vikao vya baraza la madiwani.
Mnzava alisema kuwa mwaka 2025 VETA Moshi ilitoa mafunzo ya urasimishaji wa ujuzi wa udereva kwa vijana wa bodaboda na bajaji, ambapo vijana 168 walihitimu na kupatiwa leseni rasmi za udereva.
Aidha alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kugharamia mafunzo hayo kwa kuwachangia kila kijana shilingi elfu thelathini, akisema kwa sasa vijana hao wamejiajiri, wanatambulika rasmi na wameanzisha SACCOS yao.
Naye Mwakilishi wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Francis Shio, alisema viongozi wataendelea kuelimisha jamii umuhimu wa kuwapeleka vijana katika vyuo vya ufundi na amali, akibainisha kuwa elimu ya ufundi ni fursa muhimu ya maendeleo na ajira kwa vijana.







