ZAIDI YA MITI 200 YAPANDWA KITUO CHA AFYA KISANGARA KUKUZA UOTO NA AFYA YA JAMII

KISANGARA-MWANGA.

Taasisi isiyo ya kiserikali ya Al Bayanu ECO Services Limited imeanzisha kampeni ya kijani inayolenga usafi wa mazingira na upandaji wa miti katika vituo vya afya wilayani Mwanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na urejeshaji wa uoto wa asili.

Akizungumza Mei 10, 2025, katika zoezi la usafi na upandaji miti lililofanyika katika Kituo cha Afya Kisangara, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Abdalla Lusingu Mashombo, alisema ni muhimu kwa wananchi kuanza kujenga utamaduni wa kupanda na kutunza miti kwa manufaa ya sasa na ya baadaye.

“Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, wananchi wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika upandaji wa miti na utunzaji wa misitu, hii ni hatua muhimu kwa maendeleo endelevu,” alisema Mashombo.

Mashombo alibainisha kuwa miti inayopandwa, hasa ya matunda kama miparachichi, michungwa na mipapai, pamoja na miti ya kivuli, inaweza kutoa faida kubwa kwa familia na jamii kwa ujumla.

Aliongeza kuwa taasisi hiyo ina mpango wa kutembelea hospitali na vituo vyote vya afya wilayani humo kwa ajili ya kutoa elimu ya mazingira sambamba na kufanya usafi na kupanda miti.

“Tutazunguka maeneo yote haya na pia kuhamasisha wananchi kushiriki Mwanga Marathon itakayofanyika Julai 6, 2025, kama njia ya kuimarisha afya na kuendeleza jitihada za kulinda mazingira,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mwanga Marathon and Festival, Frida Mberesero, alisema zoezi hilo la mazingira lilihusisha taasisi mbalimbali, viongozi wa vijiji, kata, pamoja na wananchi, shughuli zilizofanyika ni pamoja na kufyeka nyasi, kupanda miti na kusafisha mazingira ya Kituo cha Afya Kisangara.

“Taasisi zilizoshiriki ni pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) – Wilaya ya Mwanga, KIWAMWAKU Foundation, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mwanga, pamoja na Madiwani na Watendaji wa vijiji,” alisema Mberesero.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika Mwanga Marathon, ambayo itajumuisha mbio kwa watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 10, mbio za watu wazima (fun run), kilomita 10, 21 na 42.

Naye Mkurugenzi wa KIWAMWAKU Foundation, Ezekiel Dembere, alisema wao pia wameungana na TFS katika kupanda miti katika Kituo cha Afya Kisangara ili wagonjwa wawe na maeneo ya kupumzika wanapohudumiwa.

Kwa upande wake, Askari wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Innocent Tanya, alieleza kuwa TFS inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika juhudi za uhifadhi.

“Leo tuko hapa Kisangara kwa kushirikiana na Mwanga Marathon, ambao ni wadau wakubwa wa utalii na mazingira katika wilaya hii,” alisema Tanya.

Katika zoezi hilo, zaidi ya miti 200 ilitolewa na TFS Wilaya ya Mwanga na kupandwa kuzunguka Kituo cha Afya Kisangara.














Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.