KIWAMWAKU KUANZISHA MRADI WA HEWA UKAA KITUO CHA AFYA KISANGARA

KISANGARA-MWANGA

Taasisi isiyo ya kiserikali ya KIWAMWAKU, imesema inaendelea na jitihada za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kupitia uhamasishaji wa utunzaji wa mazingira na matumizi bora ya rasilimali asilia.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo Ezekiel Dembere aliyasema hayo jana wakati akizungumza katika mahojiano maalum na waandidhi wa habari, wakati wa zoezi la upandaji miti katika kituo cha Afya Kisangara kilichopo Kata ya Lembeni halmashauri ya Wilaya ya Mwanga mkoani hapa.

Mkurugenzi wa taasisi isiyo kuwa ya kiserikali ya KIWAMWAKU, Ndg. Ezekiel Dembere, akiwa ameshika mti kwa ajili ya kuupanda katika Kituo cha Afya Kisangara kilichopo Kata ya Lembeni Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga.

Dembere alisema taasisi yake imepanga kutekeleza mradi wa kutengeneza uzio wa miti kuzunguka Kituo cha Afya Kisangara, hatua itakayosaidia kituo hicho kuanza kuvuna hewa ukaa (carbon credits) baada ya kipindi cha takriban miaka miwili.

“Kituo cha Afya Kisangara kina uwezo wa kupata mapato ya kati ya Sh milioni 2 hadi 3 kwa mwaka kupitia uvunaji wa hewa ukaa, fedha ambazo zinaweza kusaidia kugharamia bili za umeme na maji,” alisema Dembere.

Alifafanua kuwa tayari taasisi hiyo imeshawasaidia wakulima zaidi ya 360 katika maeneo mbalimbali kupanda miti na kuanza safari ya uvunaji wa hewa ukaa katika mashamba yao.

“Kama wakulima wameshafanikisha hili, basi ni muhimu na Kituo cha Kisangara kuanza mchakato wa kupanda miti kama fensi ya mazingira, hii si tu inalinda mazingira, bali pia inaleta faida ya kiuchumi kwa taasisi za huduma kama hospitali,” aliongeza.

Mbali na masuala ya mazingira, KIWAMWAKU pia imekuwa ikishirikiana na umoja wa waendesha bodaboda katika kampeni za kupambana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mipira ya kondomu.

“Tunaamini kuwa elimu ya afya na mazingira inapaswa kwenda sambamba, tumeendelea kutoa hamasa kwa jamii kuhakikisha wanajikinga dhidi ya maambukizi mapya ya VVU, huku pia wakijali afya ya mazingira wanamoishi,” alisema Dembere.

Alihitimisha kwa kuwasihi wananchi waendelee kupanda miti na kuitunza kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.