PROF. NDAKIDEMI ASHAURI SELIMUNDU ITIBIWE BURE

BUNGENI-DODOMA.

Mbunge wa Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameiomba Serikali kuona namna ya kutoa huduma ya matibabu bure kwa wagonjwa wa selimundu.

Akiuliza swali Bungeni jijini Dodoma Mei 16,2025 Mbunge huyo alisema, gharama za matibabu za ugonjwa huo ni kubwa na wananchi wengi hawawezi kuzimudu.

“Naipoongeza Serikali inavyopambana na ugonjwa wa Selinundu, ugonjwa huu unaenea sana maeneo ya Kanda ya Ziwa, Kanda ya kati na maeneo mengine nchini, na gharama za kutibu ugonjwa huu ni kubwa sana na wananchi hawawezi kumudu, Je? Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wananchi wanatibiwa bure.? ”amehoji Prof.Ndakidemi.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel alianza kwa kumpongeza Prof. Ndakidemi kwa kuwa mtetezi wa wananchi katika Jimbo la Moshi Vijijini na kwamba tangu jimbo hilo lianzishwe haijawahi kupata mtetezi kama yeye.

“Kwanza nimjibu Mbunge Bingwa wa Moshi Vijijini ambaye tangu Jimbo hilo lianzishwe haijawahi kupata mtetezi mzuri kama Ndakidemi “alisisitiza Dkt. Mollel

Kuhusu swali la Mbunge Ndakidemi, alisema eneo la ugonjwa wa selimundu ni moja ya eneo ambalo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza hapa nchini.

“Rais ameleta teknolojia ambayo mgonjwa anatibiwa na anapona kabisa ambapo mpaka sasa watoto 30 wameshatibiwa na bila malipo”alisema Dkt. Mollel.

Aidha Dkt. Mollel alisema, nchi inapoelekea kwenye bima ya afya kwa wote pia itakuwa sulushisho la matibabu ya ugonjwa huo.

Ugonjwa wa selimundu unatajwa kuwa ni mojawapo ya changamoto kubwa za kiafya zinazowakumba watoto na vijana nchini Tanzania, hasa katika maeneo yenye idadi kubwa ya watu wa asili ya Kiafrika.

ugonjwa wa selimundu ni hali ya kurithi inayobadilisha umbo la seli nyekundu za damu, kutoka katika hali ya kawaida ya duara kuwa na umbo la hilali (au ndizi), hali inayosababisha matatizo katika mzunguko wa damu na usambazaji wa oksijeni mwilini.

“Watoto wanaoishi na ugonjwa huu hukumbwa na matatizo ya kiafya kama vile upungufu wa damu wa muda mrefu, maumivu ya ghafla, macho ya manjano, na uchovu sugu, hali hizi huathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya watoto shuleni na katika maisha ya kila siku.

Kwa mujibu wa tafiti za kisayansi, seli zilizoathirika huwa ngumu na hushindwa kupita kwa urahisi kwenye mishipa midogo ya damu, jambo linalosababisha kuziba kwa mishipa, maumivu makali, na wakati mwingine kuharibu baadhi ya viungo vya mwili. 

Sababu zinazoweza kusababisha kuibuka kwa dalili kali ni pamoja na maambukizi, upungufu wa maji mwilini, na uchovu kupita kiasi.

Ingawa hakuna tiba ya moja kwa moja ya ugonjwa wa selimundu, huduma bora za kiafya zinaweza kusaidia kudhibiti dalili na kuboresha maisha ya waathirika.

Inaelezwa kuwa uelewa wa jamii kuhusu ugonjwa huu bado ni mdogo, hivyo ni wajibu viongozi na wanajamii kuhakikisha wanatoa elimu na kusaidia familia zilizoathirika.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.