MOSHI-KILIMANJARO.
Tamasha kubwa la maonesho ya magari ya zamani lijulikanalo kama Kilimanjaro Classic Car Show and Adventurer Trip 2025 linatarajiwa kufanyika Novemba 28, mwaka huu katika viwanja vya Posta mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Mkurugenzi wa African Sports Agency Company Ltd, Joseph Mselle, ameyasema hayo Novemba 27, 2025 mjini Moshi, wakati akizungumza waandishi wa habari kuhusiana na uzinduzi wa tamasha hilo.
Mselle, amesema uzinduzi huo utakuwa mwanzo wa maandalizi ya tamasha hilo kubwa litakalofanyika mwezi Desemba 28,29 na 30 mwaka huu katika viwanja vya Mashujaa.
Amesema tamasha hilo linatarajiwa kuvutia wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na mikoa jirani, hususan kuelekea msimu wa likizo ya mwezi disemba, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Mkoa huo, kuwa mwenyeji wa maonesho ya aina hiyo.
"Maandalizi ya uzinduzi wa Tamasha la maonesho ya magari ya zamani, lijulikanalo kama Kilimanjaro Classic Car Show and Adventurer Trip 2025, yamekamilika na uzinduzi huu, utafanyika kesho Novemba 28 katika viwanja vya Posta, mjini Moshi."amesema.
Mselle amesema utalii wa magari ya zamani ni fursa mpya itakayoongeza chachu ya kukuza utalii wa ndani kwenye mkoa wa Kilimanjaro, zaidi ya ule wa Mlima Kilimanjaro unaotambulika duniani.
Kwa upande wake Mkurugenzi mwenza wa tamasha hilo Abeid Adam, amesema kuwa malengo ya tamasha hilo ni kutangaza utalii wa ndani na kudumisha mila na tamaduni za Mwafrika.
Aidha, amewaomba wananchi wote wenye magari ya zamani kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika tamasha hilo, ikiwa ni pamoja na kuyaleta magari yao kesho katika viwanja vya Posta kwa ajili ya uzinduzi.
"Wananchi wote wanakaribishwa kesho kuja kujionea maandalizi na kupokea taarifa za kina kuhusu ratiba nzima ya tamasha hili."amesema Adam.





