MOSHI-KILIMANJARO.
Katika msimu wa 2025/26 wa mvua za vuli, Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imegawa jumla ya miche 944,500 ya kahawa kwa halmashauri sita (6) za mkoa wa Kilimanjaro.
Hayo yalibainishwa jana na Afisa Kilimo wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Said Ng’ombo, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema kuwa hadi sasa miche yote iliyopangwa kwa ajili ya mkoa huo imegawiwa kwa halmashauri husika, ambapo kila halmashauri imeelekezwa kuchukua miche hiyo kutoka kwenye vitalu vilivyoandaliwa.
Aidha, alifafanua kuwa AMCOS ndizo zitatakiwa kusimamia mgawanyo wa miche hiyo kwa wakulima ili kuendeleza zao la kahawa katika mkoa wa Kilimanjaro.
Katika hatua nyingine, wakulima wameshauriwa kutumia mbolea kwa usahihi ili kuepuka upotevu wa fedha unaotokana na matumizi makubwa yasiyo ya lazima.
Ng’ombo alieleza kuwa matumizi sahihi ya mbolea yanawezesha mkulima kupata mavuno yaliyotarajiwa bila kuongeza gharama zisizo za lazima.
“Tunashauri wakulima kabla ya kununua mbolea wakutane kwanza na mtaalam wa kilimo ili kupata ushauri sahihi kuhusu aina na kiwango cha mbolea kinachohitajika kwenye mashamba yao," alisema.
Aidha, alieleza kuwa wakulima wameendelea kupatiwa elimu mbalimbali kupitia wataalamu kutoka Bodi ya Kahawa, Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI), pamoja na maafisa ugani wa halmashauri za wilaya ili kuboresha uzalishaji wa kahawa.
Ng’ombo alisema matarajio ya bodi ni kuona uzalishaji wa kahawa unaongezeka kutoka tani 5,000 za sasa hadi kufikia tani 8,000.

