DK. FRANK AWAONDOLEA HOFU WANAWAKE, KUNYONYWA MATITI SI CHANZO CHA SARATANI YA MATITI


MOSHI-KILIMANJARO.


DAKTARI kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya Kilimanjaro (KCMC), kitengo cha utafiti cha KCRI, Frank Evance, amewaondoa hofu wanawake kuhusu imani potofu kwamba kunyonya matiti kwa mwanaume kunaweza kuwasababishia kupatwa saratani ya matiti.

Hayo aliyasema Jumatano Machi 4,2026 wakati akiwasilisha mada ya ugonjwa wa saratani ya matiti katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyoandaliwa na UWT Wilaya ya Moshi Mjini na kufanyika katika Kituo cha Afya Pasua, Manispaa ya Moshi mkoani hapa.

Dk. Evance alisisitiza kuwa tafiti mbalimbali zimebaini kuwa hakuna uhusiano wowote kati ya kunyonya matiti kwa wanaume na saratani ya matiti kwa wanawake.

Alisema hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha kuwa mwanaume anaponyonya matiti ya mwanamke wakati wa faragha, awe mume au mpenzi, anaweza kuongeza hatari ya mwanamke kupata saratani ya matiti na kuwataka, wananchi kupuuza taarifa zisizo sahihi zinazosambaa mitandaoni na katika jamii kuhusu suala hilo.

Kwa mujibu wa daktari huyo, tafiti zinazoendelea zinaonesha kuwa changamoto ya saratani ya matiti bado ni kubwa, hasa kwa wanawake wenye umri kuanzia miaka 50 na kuendelea pamoja na wale wenye uzito mkubwa.


Akizungumzia utafiti wa uchunguzi wa saratani ya matiti unaofanyika mkoani Kilimanjaro, Dk. Evance alisema uchunguzi huo unawahusisha wanawake kuanzia umri wa miaka 30 na kuendelea, ukiendeshwa katika vituo vitano vya afya mkoani humo.

Alieleza kuwa matokeo ya awali yanaonesha kuwa kati ya wanawake 20 hadi 30 wanaofanyiwa uchunguzi, mmoja hupatikana na viashiria vya saratani ya matiti.

“Wengi wa wanaobainika kuwa na viashiria ni wale wenye umri mkubwa, kuanzia miaka 50 na kuendelea, pamoja na wenye uzito mkubwa, jambo ambalo linaashiria kuwa tatizo bado ni kubwa na linahitaji uelewa na hatua za mapema,” alisema Dk. Evance.

Aidha, alibainisha kuwa bado uelewa kuhusu dalili na umuhimu wa uchunguzi wa mara kwa mara ni mdogo kwa baadhi ya wanawake, wengi wao hujitokeza hospitalini pale wanapogundua dalili, badala ya kufanya uchunguzi wa kinga mara kwa mara.

"Wito kwa wanawake kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kugundua mapema dalili zozote za saratani ya matiti, kwani matibabu huwa na mafanikio zaidi endapo ugonjwa utagundulika katika hatua za awali."alisema.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Moshi akiwemo Esther Shayo, Nesia Nyagawa na Jesca James walisema wanaponyonywa matiti na wapenzi wao wakati wa faragha hujisikia raha na kuburudika zaidi, huku baadhi wakieleza kuwa tendo hilo huwasaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuwafanya kuwa huru zaidi kimahusiano.

Naye mkazi wa Shirimatunda Japhet Mpande alisema kunyonya matiti ya mwenza wake ni sehemu muhimu ya mapenzi kwao, akieleza kuwa haoni ukamilifu wa tendo la ndoa bila kushirikisha sehemu hiyo ya mwili kama ishara ya mapenzi na ukaribu.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.