MOSHI-KILIMANJARO.
MBUNGE Moshi Mjini, Ibrahim Mohamed Shayo, amesema ajali ya gari aliyopata hivi karibuni ilikuwa ni mtihani wa Mungu na siyo tukio lililosababishwa na mkono wa mtu kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidai.
Shayo aliyasema hayo leo Jumamosi, Machi 7, 2026, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wananchi uliofanyika katika uwanja wa vumbi wa standi ndogo ya mabasi mjini Moshi.
Akizungumzia tukio hilo, Shayo alisema kumekuwa na maneno mengi kuhusu chanzo cha ajali hiyo, lakini ukweli ni kwamba tairi la mbele upande wa dereva lilipasuka pamoja na rimu yake, hali iliyosababisha gari kupoteza mwelekeo na kutoka barabarani kisha kuanguka.
“Gari ilikuwa katika mwendo wa takribani kilomita 160 kwa saa, hivyo lilipotoka barabarani lililazimika kuanguka. Sasa mkono wa mtu umetoka wapi hapo?” alihoji.
Alisema anaamini tukio hilo lilikuwa ni mtihani kutoka kwa Mwenyezi Mungu na anamshukuru kwa kumuokoa na kumrudisha salama.
“Ninamshukuru Mungu kwa kuninusuru na ajali ile na kunirejesha, kwa sababu alijua wananchi wa Jimbo la Moshi Mjini walionichagua na bado kuna kazi haijaisha,” alisema Shayo.
Aliongeza kuwa anaamini Mungu amempa nafasi nyingine ili akamilishe ahadi alizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
“Mwenyezi Mungu amenirejesha ili nije kumalizia kazi za wananchi nilizowaahidi wakati wa kampeni,” alisema.
Shayo alisema miongoni mwa ahadi alizotoa ni kusimamia ujenzi wa standi mpya ya mabasi ya Ngangamfumuni, hospitali ya wilaya, uwanja wa ndege, uboreshaji wa barabara za pembezoni pamoja na ufungaji wa taa za barabarani.
Alisisitiza kuwa jukumu la mbunge ni kuwatumikia wananchi wote bila kujali makundi au majungu.
“Ndugu zangu wananchi, kazi ya mbunge si kuendekeza makundi na majungu, kazi ya mbunge ni kuwatumikia wananchi wote,” alisema.
Mbunge huyo alipata ajali ya gari Februari 18, 2026 katika eneo la Kirinjiko, wilayani Same. Wakati wa tukio hilo alikuwa katika msafara wa Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, wakitoka Same kuelekea Wilaya ya Mwanga kwa ajili ya ziara ya kikazi.














