MANISPAA YA MOSHI YAPOKEA SH BILIONI 8.1 KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO

MOSHI-KILIMANJARO. 

HALMASHAURI Manispaa ya Moshi imepokea jumla ya Sh bilioni 8.1 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka wa fedha 2025/2026.

Taarifa hiyo imetolewa Machi 7,2026 na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, wakati akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025 mbele ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Moshi Mjini.

Mnzava alisema kati ya fedha hizo, sh bilioni 2.4 ni mapato ya ndani ya halmashauri, sh bilioni 5.4 zimetoka serikali kuu na sh milioni 225.6 zimetolewa na wafadhili.

Alifafanua kuwa fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, mifugo, teknolojia, utumishi pamoja na uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Akizungumzia sekta ya afya, Mnzava alisema katika kipindi hicho sekta hiyo ilipokea sh milioni 100 kwa ajili ya kununua bidhaa za afya ikiwemo dawa, vifaa tiba pamoja na vitendanishi kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya.

Aliongeza kuwa fedha hizo pia zilitumika kununua mashine ya kisasa ya kutoa dawa za usingizi ili kuboresha huduma katika chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya Pasua, pamoja na ununuzi wa vifaa vya huduma za tiba viungo katika Kituo cha Afya Shirimatunda.

Aidha alisema Manispaa ya Moshi inaendelea kutoa huduma kupitia jumla ya vituo vya afya 72, vikiwemo vituo 49 vya huduma za afya ya msingi na kliniki 23. Pia alibainisha kuwa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi umefikia asilimia 55.

Katika sekta ya elimu ya sekondari, Mnzava alisema katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025 Manispaa ilipokea jumla ya sh bilioni 1.2, ambapo kati ya fedha hizo sh milioni 70 ni mapato ya ndani na sh bilioni 1.3 zimetoka serikali kuu pamoja na wafadhili.

Kwa upande wa elimu ya msingi, alisema katika kipindi hicho Manispaaya ilipokea jumla ya sh milioni 906.8, ambapo sh milioni 37.9 ni mapato ya ndani na Sh milioni 868.9 zimetoka serikali kuu pamoja na wafadhili.

Katika sekta ya utawala, Mnzava alisema halmashauri ilipokea sh milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi katika majengo ya ghorofa, huku ujenzi wake ukiendelea.

Alisema halmashauri itaendelea kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha hizo ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kuwanufaisha wananchi wa Manispaa ya Moshi.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.