SERIKALI YAITAKA MUWSA KUWEKA ALAMA MAENEO YENYE MIUNDOMBINU YA MAJITAKA

 


MOSHI-KILIMANJARO

SERIKALI imeitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) kuhakikisha maeneo yote yanayopitiwa na mradi wa mfumo wa majitaka yanawekewa alama maalumu ili kuonesha wazi kuwa ni maeneo ya miundombinu ya majitaka na kuzuia wananchi kuvamia na kujenga makazi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025 mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Moshi Mjini.

Mnzava alisema kumekuwepo na baadhi ya maeneo ambapo wananchi wamevamia na kujenga nyumba zao juu ya njia za bomba kuu la mfumo wa majitaka, hali inayosababisha miundombinu hiyo kuharibika na kuathiri utoaji wa huduma.

Alisisitiza kuwa uwekaji wa alama maalumu katika maeneo hayo utasaidia kuwalinda wananchi dhidi ya ujenzi holela pamoja na kulinda miundombinu ya majitaka iliyowekwa na serikali kwa gharama kubwa.

Aidha, aliwataka madiwani katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na mfumo wa majitaka kufanya sensa ya kaya ambazo hazina huduma hiyo ili kubaini mahitaji halisi ya wananchi.

Alisema taarifa hiyo itawasilishwa kwa mamlaka husika ili kuwezesha serikali kupanga namna ya kupeleka huduma hiyo kwa haraka.

Wakichangia taarifa ya utekelezaji wa ilani, baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Moshi Mjini walieleza kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazohusiana na huduma za majitaka na maji safi katika maeneo yao.

Akizungumza katika kikao hicho, Diwani wa Kata ya Kiusa, Khalid Shekoloa, alisema katika mtaa wa Police Line kuna zaidi ya nyumba 80 ambazo hazijaunganishwa na mfumo wa majitaka, licha ya kuandika barua mara kadhaa kwa MUWSA kuomba huduma hiyo.

Alisema wakati wa mvua uchafu hutiririka hadi kwenye makazi ya wananchi na kuelekezwa hadi katikati ya Mji wa Moshi pamoja na maeneo ya masoko, hali ambayo ni hatari kwa afya ya wananchi.

“Tunaiomba MUWSA kulifanyia kazi suala hili kwa haraka ili kuondoa hatari ya magonjwa kwa wananchi,” alisema Shekoloa.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Korongoni, Issa Juma, alisema baada ya MUWSA kufikisha mfumo wa majitaka katika kata hiyo, miundombinu iliyojengwa imeacha changamoto kwa wananchi kutokana na barabara kuchimbwa na kutorejeshwa katika hali yake ya awali.

Naye Diwani wa Kata ya Kaloleni, Nasibu Mariki, alisema wananchi wa kata hiyo wamekosa huduma ya maji safi kwa zaidi ya mwezi mmoja na wanalazimika kutembea umbali wa takribani kilometa mbili kufuata maji katika chemchemi.

Diwani wa Kata ya Longuo ‘B’ ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Moshi, Benedict Mwashambwa, alisema changamoto ya maji katika kata hiyo imekuwa kubwa kiasi kwamba wananchi wanapata maji mara moja tu kwa wiki.

Akijibu hoja zilizotolewa na wajumbe hao, Meneja Msimamizi wa Miundombinu ya Majitaka na Usafi wa Mazingira wa MUWSA, Mhandisi Philbert Nyangwe, alisema baadhi ya maeneo ambayo bomba kuu la majitaka linapita yamevamiwa na wananchi waliovamia na kujenga makazi yao juu ya miundombinu hiyo.

Alisema mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa na wananchi kuhakikisha miundombinu ya majitaka inalindwa ili huduma hiyo iweze kutolewa kwa ufanisi.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.