MANISPAA YA MOSHI KUSIMIKA TAA MPYA 250, KUIMARISHA USALAMA, UCHUMI WA USIKU

Alhaji Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo (kushoto),  wakipongezana na Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini Alhaji Ibrahim Mohamed Shayo.

MOSHI-KILIMANJARO.

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, amesema kuwa Manispaa hiyo inatarajia kusimika jumla ya taa 250 katika barabara na mitaa mbalimbali ili kuboresha mwanga wakati wa usiku na kusaidia kudhibiti vitendo vya uhalifu.

Amesema kati ya taa hizo, taa 150 ni mpya zitakazosimikwa, huku taa 100 zilizopo zikifanyiwa ukarabati ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Kidumo alitoa kauli hiyo Jumamosi Machi 7, 2026 alipokuwa akipewa nafasi na Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Amosi Shimba, kuwasalimia wananchi katika mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, mkutano uliandaliwa kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa mwakilishi wao bungeni.

Alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, Manispaa ya Moshi imepanga kusimika zaidi ya taa 200 mpya katika kata na mitaa mbalimbali, ikiwemo kuanzia barabara ya YMCA hadi barabara ya mzunguko wa Standi ya Mboya.

Aidha, alieleza kuwa taa hizo pia zitawekwa katika barabara ya mzunguko wa saa ya Moshi Mjini, barabara ya Nelson Mandela hadi mtaa wa Msikiti wa Riadha, hatua itakayowezesha wafanyabiashara wadogo kufanya shughuli zao kwa saa 24.

Alisisitiza kuwa mpango huo utasaidia kuimarisha ulinzi na kuboresha mandhari ya mji wa Moshi.

Katika hatua nyingine, Kidumo alisema Manispaa imeongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 kutoka shilingi bilioni 6 hadi kufikia shilingi bilioni 12.

Alifafanua kuwa fedha hizo zitatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya masoko, standi ya mabasi pamoja na kuboresha usafi wa mazingira ya mji wa Moshi, ikiwemo ununuzi wa gari la kubeba taka.

Aidha, Kidumo aliwataka madiwani na viongozi wengine wa wananchi kuzingatia utekelezaji wa ahadi walizozitoa wakati wa kampeni.

“Kwa sasa tumeshamaliza siasa, wananchi wanachotarajia kutoka kwetu ni kuona maendeleo na utekelezaji wa ahadi tulizozitoa wakati wa kampeni katika kila kata, madiwani twendeni tukayatekeleze, kwani wananchi walituchagua wakiamini tutayafanya,” alisema.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.