MOSHI-KILIMANJARO.
TAASISI ya Tanzania Ex-Prisoners Foundation (TEPF) imetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa mahabusu wanawake walioko Gereza la Karanga mkoani Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari.Machi 10, 2026 Mkurugenzi wa taasisi hiyo Rose Malle alisema taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine imeona ni vyema kusherehekea siku hiyo kwa kuwasaidia wanawake walioko gerezani kwa kuwapatia mahitaji muhimu.
Alisema msaada huo umejumuisha sabuni za kufulia na kuogea, taulo za kike, mashuka ya kujifunika, sukari pamoja na mafuta ya kujipaka ikiwa ni mchango wa taasisi hiyo katika kuunga mkono maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Malle alisema pamoja na misaada hiyo, taasisi yao imekuwa ikitoa elimu kwa wafungwa waliomaliza vifungo vyao ili kuwasaidia kurejea katika jamii wakiwa na ujuzi wa kujitegemea kiuchumi.
Alisema elimu wanazotoa ni pamoja na ujasiriamali na stadi za ufundi ambazo huwasaidia waliotoka gerezani kupata ajira au kujiajiri na hivyo kujikimu wao pamoja na familia zao.
Akizungumza, Diwani wa Kata ya Korongoni Issa Juma alisema ni muhimu jamii kuendelea kuelimishwa kuhusu changamoto zinazowakabili wanawake ili kupunguza matukio ya ukatili yanayoweza kusababisha migogoro katika familia na jamii.
Naye Diwani wa Kata ya Miembeni Haruna Mushi alisema ziara hiyo imewapa fursa ya kujifunza na kushuhudia juhudi zinazofanywa na mahabusu wanawake katika kujishughulisha na kazi mbalimbali za mikono wakiwa gerezani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava aliipongeza taasisi ya TEPF kwa juhudi zake za kuielimisha jamii kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha watu kuingia magerezani pamoja na kuwasaidia waliotoka gerezani kujijenga kisaikolojia na kiuchumi.
Awali akizungumza Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kilimanjaro, Mrakibu wa Polisi Asia Matauka alisema wakati mwingine watu wanaojikuta gerezani huwa wamepitia mazingira magumu ya ukatili tangu utotoni, hali inayoweza kuwafanya baadaye kujikuta wakitenda vitendo vya ukatili dhidi ya wengine.
















