WHO KUJADILI KUIPANDISHA HADHI MAABARA YA KIBONG’OTO KUWA MAABARA YA RUFAA YA KIMATAIFA YA TB

Maabara ya Usalama wa Kibaiolojia Daraja la Tatu iliyopo katika Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto (KIDH)

SIHA-KILIMANJARO.

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) liko katika mazungumzo ya kuipandisha hadhi Maabara ya Usalama wa Kibaiolojia Daraja la Tatu iliyopo katika Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto (KIDH), ili iwe Maabara ya Rufaa ya Kimataifa ya Kifua Kikuu (TB).

Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Leonard Subi, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika maabara hiyo.

Alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha uwezo wa kugundua na kufuatilia usugu wa vimelea vya kifua kikuu pamoja na kusaidia tafiti za magonjwa ya kuambukiza, jambo litakalosaidia kupunguza gharama za kutuma sampuli za uchunguzi nje ya nchi.


Shirika la Afya Duniani (WHO) liko katika mchakato wa kuitambua maabara yetu kuwa Maabara ya Rufaa ya Kimataifa ya Kifua Kikuu,” alisema Dk. Subi.

Alieleza kuwa uwepo wa Maabara ya Usalama wa Kibaiolojia Daraja la Tatu umeimarisha juhudi za kudhibiti kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza duniani, hali inayochangia kulinda afya ya binadamu pamoja na kuimarisha uchumi.

Kwa mujibu wa Dk. Subi, maabara hiyo hufanya uchunguzi wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa mbalimbali zinazotumika kutibu magonjwa, pamoja na vipimo vya kazi za ini, figo na homoni.

Pia hufanya uchunguzi wa vimelea vya magonjwa kwa kutumia mbinu za kisasa za kimolekuli na kutathmini kiwango cha dawa mwilini ili kuboresha matibabu kwa wagonjwa.

Akizungumzia tafiti, alisema maabara hiyo hutumika pia katika kufanya tafiti na ubunifu (innovation) katika sayansi ya tiba na kinga, ikiwemo ugunduzi wa dawa mpya, vitendanishi na vifaa tiba, pamoja na kuwezesha maendeleo ya chanjo na mbinu mpya za kukinga magonjwa ya kuambukiza siku zijazo.

Aliongeza kuwa maabara hiyo ina uwezo wa kuhifadhi sampuli za vimelea kwa muda mrefu hadi miaka 50, ikiwa na uwezo wa kuhifadhi hadi lita 47,000 za sampuli, na kwamba uwekezaji huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya sekta ya afya iliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, alisema maabara hiyo imepatiwa vifaa vya kisasa vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 10, ikiwemo mashine za kuchakata vimelea na vinasaba ambazo husaidia kubaini chanzo cha magonjwa pamoja na kufuatilia milipuko ya magonjwa mbalimbali. 

Aidha alisema maabara hiyo hutumika kutoa mafunzo na kujenga uwezo kwa wataalamu wa afya pamoja na wanafunzi.

Dk. Subi alieleza pia kuwa Hospitali ya Kibong’oto ilikuwa ya kwanza nchini Tanzania kubaini anuai (variants) za virusi vya Covid-19 baada ya kupokea sampuli 69 kutoka Wizara ya Afya, uchunguzi huo ulifanyika kwa kutumia kifaa maalumu chini ya usimamizi wa mwanasayansi Dk. Shaban Mziray wa hospitali hiyo.

Katika hatua nyingine, Dk. Subi alisema hospitali hiyo kupitia Maabara yake ya Afya ya Jamii Daraja la Tatu imechaguliwa kujengewa uwezo ili kufikia hadhi ya juu ya maabara ya rufaa ya kimataifa (Supra National Laboratory), na kuwa ya tano barani Afrika, huku pia ikiongoza tafiti za kupunguza muda wa matibabu kwa wagonjwa wa kifua kikuu katika nchi sita za Afrika.

Aliongeza kuwa KIDH imepiga hatua nyingine muhimu baada ya kupata ithibati ya kimataifa kutoka Taasisi ya Ithibati ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADCAS) kwa vipimo 52 vya utafiti vinavyofanyika katika hospitali hiyo.

Alisema mafanikio hayo yametambuliwa na SADCAS, taasisi inayohusika na ithibati katika sekta ya afya chini ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Utambuzi huu umetokana na miaka mingi ya kuboresha ubora wa huduma na kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wetu, pamoja na msaada mkubwa tunaoupata kutoka serikalini ambao ulitambuliwa na maofisa wa SADCAS waliotembelea hospitali yetu kwa nyakati tofauti,” alisema.

Alibainisha kuwa katika tathmini ya kwanza iliyofanyika mwaka 2018, hospitali hiyo ilipata ithibati kwa vipimo vinne; mwaka 2022 vipimo 28 vilitambuliwa, na mwaka 2024/2025 jumla ya vipimo 52 vimetambuliwa.

Kwa mujibu wa Dk. Subi, ambaye ni Daktari Bingwa wa Afya ya Jamii, alisema mafanikio hayo yalitokana na ubora wa tafiti zinazofanywa katika nyanja mbalimbali zikiwemo Kliniki ya Kemia, Serology, Mycobacteriology, Parasitology na Microbiology.

Alisema hatua hiyo imeifanya Hospitali ya Kibong’oto kuendelea kutambulika na kuheshimiwa katika uwanja wa tiba na tafiti za afya kimataifa.

“Hii ni ishara kuwa hospitali ya Kibong’oto iko tayari kukabiliana na aina yoyote ya ugonjwa wa kuambukiza, na lengo letu ni kuhakikisha kila utafiti unaofanywa hapa unafikia viwango vya kimataifa,” alisema.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.