ASKOFU MONO ATAKA UMOJA WA VIONGOZI KUCHOCHEA MAENDELEO MWANGA

MWANGA-KILIMANJARO.

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mwanga, Askofu Dk. Daniel Henry Mono, amewataka viongozi wa Wilaya ya Mwanga kuimarisha umoja na mshikamano ili kuharakisha maendeleo ya wilaya hiyo.

Askofu Mono alitoa ushauri huo Machi 11, 2026 alipokutana na Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Jeremiah Boniphace Mziray, aliyefika ofisini kwake kwa lengo la kufanya mazungumzo ikiwa ni sehemu ya ziara ya kukutana na viongozi wa dini, makundi mbalimbali ya kijamii pamoja na taasisi za serikali na binafsi.

Katika mazungumzo hayo, Askofu Mono alisisitiza umuhimu wa viongozi kushirikiana na kuunganisha nguvu zao katika kushughulikia masuala ya maendeleo na ustawi wa jamii ya Mwanga. Aidha, alishauri wadau mbalimbali washirikishwe kikamilifu katika mipango ya maendeleo ya wilaya, hususan katika jitihada za kufungua mji wa Mwanga kiuchumi.

Askofu huyo pia aliipongeza Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Mwanga kwa kutambua mchango wa taasisi za dini katika maendeleo ya jamii, akisisitiza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuendelezwa kwa manufaa ya wananchi.

Ziara hiyo imelenga kujenga mahusiano mazuri kati ya viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini na makundi mbalimbali ya kijamii, pamoja na kujadili masuala ya maendeleo yanayowahusu wananchi wa Wilaya ya Mwanga.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na baadhi ya wakuu wa majimbo wa Dayosisi ya Mwanga pamoja na Mwenyekiti wa Vijana wa Dayosisi hiyo, Joseph Mrutu, ambao kwa pamoja walipata fursa ya kujadili na Askofu masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Jeremiah Boniphace Mziray, alisema ziara hiyo inalenga kuzifikia taasisi zote zilizopo katika jimbo hilo kama sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano na kuyafikia makundi mbalimbali ya kijamii.

Aliongeza kuwa milango ya Ofisi ya Mbunge pamoja na mbunge mwenyewe iko wazi wakati wote kwa taasisi na wananchi wanaotaka kushirikiana katika kuleta maendeleo ya Mwanga.

Mziray alisema juhudi hizo zinaenda sambamba na ziara iliyofanywa hivi karibuni na Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Dk. Ngwaru Maghembe, katika kata mbalimbali za jimbo hilo kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kwa kushirikiana na wataalamu kutoka halmashauri pamoja na viongozi wa chama na serikali.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.