BARAZA LA WAFANYAKAZI KIBONG’OTO LAPITISHA RASIMU YA BAJETI YA SH BILIONI 19 KWA MWAKA WA FEDHA 2026/2027



Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Maalumu ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto (KIDH) Dk. Leonard Subi,  akizungumza katika kikao cha kupanga na kupitisha bajeti ya Mwaka 2026/2027

SIHA-KILIMANJARO.

BARAZA la Wafanyakazi la Hospitali Maalumu ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto (KIDH) limepitisha rasimu ya bajeti ya zaidi ya Sh bilioni 19 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za hospitali hiyo katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Leonard Subi, alisema hayo jana wakati wa kikao cha kupanga na kupitisha bajeti hiyo, akieleza kuwa makadirio hayo yameandaliwa kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya Kitaifa na Kisekta.

Alitaja baadhi ya miongozo iliyozingatiwa kuwa ni pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030, Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya wa mwaka 2021–2026, Sera ya Afya ya mwaka 2007 pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Dk. Subi alisema, maandalizi ya bajeti hiyo pia yamezingatia Mpango Mkakati wa Hospitali wa mwaka 2022–2026, miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kudhibiti magonjwa ya milipuko, pamoja na vipaumbele vya Wizara ya Afya na vya hospitali hiyo katika kuboresha utoaji wa huduma za afya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Katibu wa Afya katika hospitali hiyo Neema Mwakyembe Mbinga, katika kikao hicho, alisema bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 inatarajiwa kufikia zaidi ya Sh bilioni 19, fedha zitakazotokana na vyanzo mbalimbali vya mapato pamoja na bajeti ya mishahara ya watumishi.

Katika mgawanyo wa bajeti hiyo, kiasi cha Sh bilioni 1.7 kinatarajiwa kupatikana kutoka vyanzo vya ndani vya mapato ya hospitali, ikiwemo malipo ya papo kwa papo na makusanyo kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Aidha, alosema Serikali Kuu inatarajiwa kuchangia Sh bilioni 2.22 kwa ajili ya matumizi ya kawaida (OC), huku Sh bilioni 5 zikitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Sh bilioni 2 kutoka katika miradi ya tafiti.

Kwa upande wa mishahara ya Watumishi, bajeti imekadiriwa kufikia Sh bilioni 6.41, wakati Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh bilioni 1.67 kupitia taasisi mbalimbali, ikiwemo Global Fund, LHL International na USAID Afya Yangu kupitia EGPAF.

Hospitali hiyo pia inatarajia kupokea dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Sh bilioni 1.08 kupitia Bohari ya Dawa (MSD), ambapo uongozi wa hospitali hiyo, umeeleza kuwa utekelezaji wa bajeti hiyo utasaidia kuimarisha utoaji wa huduma za kinga, uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya kuambukiza, sambamba na kuboresha miundombinu na huduma kwa wagonjwa.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.