MOSHI-KILIMANJARO.
MKUU wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kilimanjaro, Mrakibu wa Polisi (SP) Asia Matauka, amewataka wazazi kuhakikisha shughuli za kutafuta kipato haziwatenge na watoto wao, akisisitiza kuwa uwajibikaji wa familia ni muhimu katika kuwasaidia watoto kueleza changamoto wanazopitia.
SP Matauka alitoa rai hiyo jana mjini Moshi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ongezeko la matukio ya ukatili katika jamii, akibainisha kuwa ukaribu kati ya mzazi na mtoto ni silaha muhimu ya kugundua na kuzuia vitendo vya ukatili mapema.
Alisema wazazi wanapojenga mahusiano mazuri na watoto wao na kuwafanya kuwa marafiki wa karibu, huwa rahisi kwa watoto hao kueleza matatizo wanayokutana nayo katika maisha ya kila siku.
“Mara nyingi mzazi anapokuwa mbali na familia yake, mtoto hushindwa kuwa huru kueleza changamoto anazopitia, ndiyo maana wakati mwingine mwalimu ndiye anayegundua mtoto amefanyiwa ukatili huku mzazi wake akiwa hajui chochote kutokana na kutokuwa karibu naye,” alisema SP Matauka.
Alieleza kuwa baadhi ya wazazi, hasa akina mama, wamekuwa wakijikita zaidi katika shughuli za kutafuta kipato kiasi cha kupunguza muda wa kukaa na watoto wao, hali inayosababisha watoto kukosa nafasi ya kueleza matatizo wanayokumbana nayo.
Kwa mujibu wa SP Matauka, baadhi ya akina mama wamekuwa wakijihusisha na vikundi vya kifedha kama vile VICOBA na vibati, ambapo wakati mwingine changamoto za marejesho ya fedha huleta msongo wa mawazo unaoweza kuathiri mahusiano ndani ya familia.
Alisema katika mazingira kama hayo, mtoto anapojaribu kueleza kuwa amefanyiwa ukatili au ameumizwa shuleni au njiani, mzazi anaweza kushindwa kumsikiliza kutokana na msongo wa mawazo na hivyo mtoto kubaki na maumivu yake peke yake.
Aidha, SP Matauka alisema matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto katika Mkoa wa Kilimanjaro hutokea ndani ya familia, akitolea mfano baadhi ya visa ambapo baba mzazi humfanyia ukatili wa kingono mtoto wake.
Alisema wakati mwingine akina mama hushindwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria kwa kuhofia athari za kifamilia na kiuchumi iwapo baba wa watoto atachukuliwa hatua za kisheria.
“Mama anaweza kusema nina watoto sita na wote nimezaa na baba huyu; nikitoa maelezo polisi na akafungwa, watoto wataishije wakati sina kipato chochote,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wazazi na jamii kwa ujumla kuweka mbele maslahi ya watoto, kujenga mawasiliano ya karibu ndani ya familia na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria ili kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.








