BOLT YAIMARISHA USHIRIKIANO NA LATRA KUKUZA USAFIRI WA MTANDAO

DAR ES SALAAM.

KAMPUNI ya usafiri wa mtandao ya Bolt Tanzania imekutana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) pamoja na Kikosi cha Usalama Barabarani kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika kusimamia na kukuza sekta ya usafiri wa mtandao nchini.

Meneja Mkuu wa Bolt Afrika Mashariki, Dimmy Kanyankole, aliyasema hayo jana Machi 12, 2026 wakati wa mazungumzo katika kikao hicho, ambapo alisema lengo la kampuni hiyo ni kushirikiana kwa karibu na LATRA ili kuhakikisha ukuaji wa sekta unaenda sambamba na uzingatiaji wa sheria.

Kikao hicho cha ngazi ya juu kililenga kujadili masuala mbalimbali ya udhibiti, uzingatiaji wa sheria na changamoto zinazoikabili sekta hiyo, pamoja na kubaini suluhu za vitendo zitakazochochea ukuaji endelevu na ushiriki mpana wa wadau.

Katika kikao hicho, Bolt iliwasilisha mkakati wake wa soko wa mwaka 2026 unaolenga kuongeza idadi ya madereva na abiria kwa takriban asilimia 40. Mkakati huo pia unahusisha kuanza rasmi huduma zake Zanzibar pamoja na kupanua wigo wa huduma katika miji mingine ya Tanzania Bara.

"Kwa sasa Bolt inatoa huduma katika miji minane nchini, ikiwemo Mwanza, Morogoro, Mbeya na Tanga, huku kampuni hiyo ikieleza kuwa inaendelea kutafuta fursa za kuongeza maeneo mapya ya huduma kadri mahitaji yanavyoongezeka."alisema

Kanyankole, alisema ili kuimarisha ushiriki wa madereva katika mfumo rasmi wa usafiri wa mtandao, Bolt imeeleza utayari wake wa kushirikiana kwa karibu na mamlaka za udhibiti ili kurahisisha upatikanaji wa leseni za kibiashara kwa madereva wanaotumia majukwaa ya kidijitali.

Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na utekelezaji wa kampeni ya pamoja ijulikanayo kama “Drive to Compliance”, itakayolenga kuongeza uelewa kwa madereva, kurahisisha mchakato wa urasimishaji na kukuza ushiriki salama na halali katika sekta hiyo kwa manufaa ya Watanzania.

Naye Mkuu wa Udhibiti na Sera wa Bolt Afrika, Weyinmi Aghadiuno, alisema kikao hicho ni sehemu ya juhudi za kampuni hiyo katika kukuza uwazi na majadiliano yanayozingatia ushahidi.

Alisema ushirikiano wa kimfumo kati ya wadau utasaidia kuimarisha uadilifu wa udhibiti, kuhakikisha uwepo wa bei za haki na kurahisisha mazingira ya kazi kwa madereva katika maeneo yote ambayo Bolt inatoa huduma.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa LATRA, Halima Lutavi, alisema mamlaka hiyo iko tayari kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha sekta ya usafiri wa mtandao inakua huku ikilinda usalama wa watumiaji, haki za madereva na mapato ya serikali.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.