NGUJINI-MWANGA.
MVUA kubwa iliyonyesha Machi 12, mwaka huu, imesababisha madhara makubwa katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Ngujini, iliyoko halmashauri ya wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, ambapo miundombinu imeharibika na wananchi kuathirika kwa kiasi kikubwa.
Hayo yamesemwa leo Machi 13,2026 na Diwani wa Kata ya Ngujini, Rodgers Msangi, wakati wa ziara ya kukagua maeneo yaliyoathirika na mvua hiyo akiwa ameambatana na Wataalamu uongozi wa Wakala ya Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), Wilayani humo, ili kujionea hali halisi na kutafuta hatua za haraka za kuchukua.
Alisema kutokana na mvua hiyo, sehemu kubwa ya barabara ya Kisangara kuelekea Ngujini kupitia Shighatini imeharibika vibaya, hali iliyosababisha usafiri kuwa mgumu kwa wananchi wanaotumia njia hiyo.
Aidha, alisema barabara ya kuelekea Mringeni kutoka Chanjale haipitiki kabisa, baada ya majabali na vifusi kujaa barabarani kiasi kwamba haviwezi kuondolewa kwa mikono.
"Leo nimefika na kutembelea maeneo yote yaliyoathirika pamoja na Wataalamu wa TARURA ili kuona nini kifanyike haraka kurejesha miundombinu na kusaidia wananchi walioathirika,” alisema Msangi.
Mbali na kuharibu barabara, mafuriko hayo pia yamesomba mabomba ya maji, na kusababisha maeneo ya Lembeni, Kisangara Chini pamoja na Ustawi wa Jamii kukosa huduma ya maji.
"Baadhi ya vijiji, athari zimekuwa kubwa zaidi ambapo baadhi ya nyumba za wananchi zimefukiwa na vifusi vya udongo, hasa katika vijiji vya Chanjale, Mringeni na Ngujini."alisema Msangi.
Aliongeza kuwa tathmini inaendelea kufanyika ili kubaini kiwango cha uharibifu na kupanga mikakati ya kurekebisha barabara pamoja na kurejesha huduma muhimu kwa wananchi.











