SIHA-KILIMANJARO.
KATIKA kuelekea maadhimisho ya wiki ya Kifua Kikuu Duniani, ambayo hufanyika kila ifikapo Machi 24 ya kila mwaka, Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH) imejipanga kuadhimisha siku hiyo kwa namna ya kipekee ndani ya viunga vya hospitali hiyo kwa kuwashirikisha wagonjwa wanaopatiwa matibabu ya kifua kikuu hospitalini hapo.
Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Afisa Ustawi wa Jamii wa hospitali hiyo, Wazoeli Mshana, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuwapa moyo wagonjwa na kuwahamasisha kuendelea na matibabu hadi kupona kabisa.
Alisema bonanza hilo litahusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, kuvuta kamba, mbio za kukimbia pamoja na mashindano ya maswali ya papo kwa papo, yote yakilenga kuwapa wagonjwa faraja na kupunguza msongo wa mawazo.
"Tumeamua kuadhimisha siku hii kupitia michezo kwa sababu michezo ni moja ya mambo yanayompa mtu utulivu wa akili na kumsaidia kupunguza msongo wa mawazo,” alisema Mshana.
Alisema katika maadhimisho hayo pia watachagua balozi kutoka miongoni mwa wagonjwa ambaye atakapopona na kurejea katika jamii ataweza kuelimisha wengine kuwa ugonjwa wa kifua kikuu unatibika na kupona kabisa.
"Tunataka kuhakikisha wagonjwa wote wanapata matibabu bora na wanapona kabisa, kwani serikali imewekeza fedha nyingi katika matibabu ya ugonjwa huu."
Aidha Mshana aliongeza kuwa hospitali hiyo inaendelea kuhakikisha wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wanapatiwa huduma bora pamoja na mazingira rafiki ya matibabu ili waweze kurejea katika maisha yao ya kawaida









