DIWANI KIUSA AKABIDHI VIFAA VYA USAFI, AWAPA MOTISHA WAFANYAKAZI WA USAFI

KIUSA-MOSHI.

DIWANI wa Kata ya Kiusa, Khalid Shekoloa, amekabidhi vifaa vya kisasa vya usafi kwa akina mama wanaojishughulisha na shughuli za usafi katika kata hiyo, iliyopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni juhudi za kuimarisha mazingira safi na salama kwa jamii.

Shekoloa aliyasema hayo jana wakati aliposhiriki kufanya usafi katika maeneo ya kata hiyo ikiwemo katika soko la ndizi Kiusa, maeneo ya gereji, na kwenye mitaro iliyopo katika kata hiyo.

Alisema vifaa alivyovika idhi ni pamoja na makoti ya kuakisi mwanga (reflector jackets) jozi mbili kwa kila mfanyakazi, mabuti, kofia ngumu (helmet), glovu pamoja na vifaa vya kuokotea taka.

Akikabidhi vifaa hivyo, Shekoloa alieleza dhamira yake ya kuhakikisha Kata ya Kiusa inakuwa kinara wa usafi nchini, akibainisha kuwa kwa sasa mtaa unaoongoza kitaifa ni mtaa wa Rengua uliopo kata ya Mawenzi.

Mbali na vifaa hivyo, diwani huyo pia aliwapatia zawadi akina mama hao ikiwa ni maandalizi ya kuelekea sikukuu za Eid na Pasaka, ili kuwawezesha kusherehekea kwa furaha pamoja na familia zao.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kiusa, Dativa Tesha, alisema kuwa awali walikuwa wakitumia vifaa vilivyotolewa na manispaa ambavyo vilikuwa vimechakaa na hivyo kuhatarisha afya na usalama wa watumiaji.

"Namshukuru sana diwani kwa kuguswa na changamoto hiyo na kutoa msaada wa vifaa vipya na salama."alisema.

Naye Bibi Afya wa kata hiyo, Mashekhe Kamota, alisisitiza umuhimu wa matumizi ya vifaa kinga wakati wa kufanya usafi, akieleza kuwa vinasaidia kuzuia maambukizi ya magonjwa yatokanayo na taka, kemikali hatarishi pamoja na mazingira machafu.

Aliongeza kuwa matumizi sahihi ya glovu, mabuti na mavazi maalum hupunguza hatari ya majeraha na magonjwa ya ngozi, hivyo kuwalinda wafanyakazi na kuboresha afya zao kwa ujumla.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Alhaji Zuberi Abdallah Kidumo, amewataka wakazi wa manispaa hiyo kuendelea kushirikiana na viongozi wa mitaa katika kuhakikisha taka zinakusanywa na kutupwa katika maeneo sahihi badala ya kutupa hovyo.

Alisisitiza umuhimu wa kutenganisha taka majumbani, akibainisha kuwa mabaki ya chakula yanapaswa kuwekwa tofauti na taka za plastiki, huku akihimiza kila familia kuwa na vyombo maalum vya kuhifadhia taka.

Aidha, Kidumo aliwataka wazazi kuwafundisha watoto wao utamaduni wa usafi na utunzaji wa mazingira tangu wakiwa wadogo.

“Usafi unaanza na mtu binafsi, tukizingatia utenganishaji sahihi wa taka na utupaji katika maeneo husika, Manispaa ya Moshi itaendelea kuwa kinara wa usafi nchini kila mwaka,” alisema Meya Kidumo.

Ikumbukwe kuwa Aprili 8, 2025, Manispaa ya Moshi ilitangazwa kushika nafasi ya kwanza kwa usafi kati ya Manispaa 19 nchini Tanzania.

Aidha, Mtaa wa Rengua uliopo Kata ya Mawenzi ulitambuliwa kuwa mtaa msafi zaidi kitaifa.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.