SIHA-KILIMANJARO.
SIKU ya Kifua Kikuu Duniani huadhimishwa kila mwaka Machi 24 ikiwa ni sehemu ya kuongeza uelewa wa kimataifa kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu (TB) na athari zake kwa afya ya umma.
Maadhimisho haya hulenga kuhamasisha jamii, serikali na wadau wa afya kuchukua hatua madhubuti katika kudhibiti na hatimaye kutokomeza ugonjwa huo.
Kauli mbiu ya mwaka 2026 isemayo “Ndiyo! Tunaweza kumaliza TB!” inaakisi matumaini na dhamira ya pamoja ya kupambana na ugonjwa huo. Kauli mbiu hii inasisitiza umuhimu wa utambuzi wa mapema, matibabu ya wakati na kupunguza unyanyapaa kwa wagonjwa wa kifua kikuu.
Historia ya siku hii inaanzia Machi 24, 1882, ambapo Dkt. Robert Koch alitangaza ugunduzi wa bakteria wanaosababisha kifua kikuu. Ugunduzi huu ulikuwa hatua muhimu katika kuelewa na kupambana na ugonjwa huo, na ndiyo sababu tarehe hiyo imekuwa alama ya mapambano dhidi ya TB duniani.
Licha ya uwepo wa tiba, kifua kikuu bado ni moja ya magonjwa hatari zaidi ya kuambukiza duniani, mamilioni ya watu huathirika kila mwaka, hasa katika nchi zinazoendelea, hali inayosisitiza umuhimu wa kuendelea na kampeni za uhamasishaji, upimaji na matibabu.
Hata hivyo, katika mazingira ya kazi kama migodini, kuna changamoto nyingine inayochangia kuenea kwa kifua kikuu, ugonjwa wa silicosis.
Ugonjwa huu wa mapafu husababishwa na kuvuta vumbi lenye chembechembe za silica, zinazopatikana katika miamba na udongo.
Silicosis ni ugonjwa sugu unaoweza kuchukua miaka 10 hadi 20 kuonyesha dalili, mara nyingi huchanganywa na kifua kikuu kutokana na kufanana kwa dalili zake kama kikohozi kikali, upungufu wa pumzi na uchovu wa mwili.
Katika migodi ya Tanzanite ya Mirerani, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wachimbaji wanakabiliwa na hatari kubwa ya kupata silicosis kutokana na mazingira yao ya kazi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wachimbaji akiwemo Bakari Hussein, Stephano Kaaya, Omari Juma, Jumbe Msele, John Lyimo na Joseph Mollel walisema wanakumbana na changamoto kubwa za kiafya.
Walieleza kuwa hukumbwa na kikohozi kikali, upungufu wa pumzi na uharibifu wa mapafu, huku wakikosa vifaa vya kujikinga kama barakoa maalumu pamoja na mifumo bora ya uingizaji hewa migodini.
Kwa upande wake, Mratibu wa Shughuli za Afya ya Jamii katika Hospitali ya Kibong’oto, Dk. Alexander Mbuya, alisema kuwa kiwango cha maambukizi ya kifua kikuu kwa wachimbaji wa Mirerani kimeongezeka mara 18 zaidi ya wastani wa kitaifa, anaeleza kuwa hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa silicosis.
“Vumbi la silica linapoingia kwenye mapafu husababisha uharibifu tishu na kuyafanya mapafu kukakamaa, hivyo kushindwa kufanya kazi yake ya kawaida,” alifafanua Dk. Mbuya.
Aliongeza kuwa shughuli za uchimbaji wa Tanzanite zinazohusisha kupasua miamba huzalisha vumbi hatarishi ambalo huingia moja kwa moja kwenye mapafu ya wachimbaji na kusababisha madhara ya muda mrefu.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, uharibifu huu wa mapafu husababisha makovu (fibrosis) na kupunguza uwezo wa kupumua, hali inayoongeza uwezekano wa mtu kupata kifua kikuu kwa urahisi zaidi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, alisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za kinga migodini.
Alisema wamiliki wa migodi wanapaswa kuhakikisha wanapunguza vumbi kwa kumwagilia maji wakati wa uchimbaji.
Aidha, aliwataka kuhakikisha wachimbaji wanapatiwa elimu ya afya, vifaa vya kujikinga na kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara ili kubaini magonjwa mapema na kuanza matibabu kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa ya Kuambukiza Kibong’oto, Dk. Leonard Subi, alisema kuwa silicosis haina tiba mara mtu anapopata ugonjwa huo.
Alieleza kuwa huduma inayotolewa ni ya kusaidia tu, ikiwemo kumpatia mgonjwa hewa ya oksijeni ili kumuwezesha kupumua vizuri zaidi.
Pia alishauri wamiliki wa migodi kuwapatia wachimbaji bima ya afya ili waweze kupata matibabu wanapohitaji.
Kwa kuhitimisha, Siku ya Kifua Kikuu Duniani ni ukumbusho muhimu wa haja ya kuunganisha juhudi za kupambana na kifua kikuu na magonjwa yanayochangia kuenea kwake kama silicosis.
Kupitia ushirikiano wa serikali, wataalamu wa afya, waajiri na jamii, inawezekana kupunguza maambukizi na kulinda afya za wananchi.
Kwa pamoja, tukizingatia elimu, kinga na matibabu sahihi, tunaweza kufikia lengo la kumaliza kifua kikuu, Hakika, Ndiyo! Tunaweza kumaliza TB!








