PBWB KUWASHIRIKISHA WANAFUNZI KULINDA VYANZO VYA MAJI

MOSHI-KILIMANJARO.

WANAFUNZI katika mkoa wa Kilimanjaro wanatarajiwa kupata fursa ya kipekee ya kujifunza na kushuhudia kwa vitendo shughuli za utunzaji wa vyanzo vya maji zinazofanywa na Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB), ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya wiki ya maji inayoanza machi 16 hadi kufikia kilele chake machi 22 mwaka huu.

Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha Watumishi kutoka vyombo vya Watumia Maji, Mameneja wa RUWASA Wilaya za mkoa wa Kilimanjaro, Menejimenti ya RUWASA mkoa, Wasimamizi wa Sekta ya Maji pamoja na Waandishi wa habari;

Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Mhandisi Segule Segule, alisema lengo la kuwashirikisha wanafunzi ni kuwajengea uelewa na kuwahamasisha kuwa walinzi wa rasilimali za maji kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Mhandisi Segule, alisema PBWB imeona kuwashirikisha wanafunzi hao kuona kwa vitendo jitihada zinazofanywa katika kulinda vyanzo vya maji, ili iwe chachu kwao kuendeleza juhudi hizo na kuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi wa mazingira.

"Tunataka vijana wetu waone kwa vitendo jitihada zinazofanywa katika kulinda vyanzo vya maji, ili iwe chachu kwao kuendeleza juhudi hizi na kuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi wa mazingira,” alisema Segule.

Alisema Kauli mbiu ya wiki ya maji mwaka huu isemayo “Rasilimali za Maji na Usawa wa Kijinsia” inayoelezea usawa katika upatikanaji wa maji, ushirikishwaji katika maamuzi na pia usambazaji wa haki wa rasilimali unaogusa jamii nzima, huku akibainisha kuwa vijana ni kundi muhimu katika kufanikisha azma hiyo.

Aidha, alifafanua kuwa sekta ya maji ina majukumu makuu mawili ambayo ni usimamizi endelevu wa rasilimali za maji pamoja na kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi.

Aliongeza kuwa katika wiki ya maji, PBWB itaendesha shughuli mbalimbali, ikiwemo utunzaji wa vyanzo vya maji, ufuatiliaji wa mwenendo wa maji katika vyanzo, usomaji wa vipimo, pamoja na usimamizi wa miundombinu ya maji.

Segule alitoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika kulinda vyanzo vya maji kwa kuepuka uchafuzi wa mazingira na kuimarisha uoto wa asili kupitia upandaji miti. 

“Kila mmoja wetu ana nafasi ya kulinda rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya taifa,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Weransari Munisi, alisema sekta ya maji ina taasisi kuu nne zinazoshughulika na huduma hiyo muhimu.

Alizitaja taasisi hizo kuwa ni RUWASA inayohusika na usambazaji wa maji vijijini, mamlaka za maji za mijini zinazosimamia huduma za maji katika miji, Bodi ya Maji Bonde Pangani ambayo ni msimamizi wa rasilimali za maji, pamoja na taasisi za Maabara zinazoshughulika na ufuatiliaji wa ubora wa maji.

Maadhimisho ya wiki ya maji hutoa jukwaa muhimu la kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa maji na wajibu wa kila mmoja katika kuyatunza kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.