MOSHI-KILIMANJARO.
MBUNGE mstaafu wa Jimbo la Moshi Mjini, Abdullfatah Priscus Tarimo, ameendelea kuonesha mshikamano na upendo kwa jamii kwa kuandaa futari maalum kwa waumini wa dini ya Kiislamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Hafla hiyo iliyofanyika kwa amani na furaha imewakutanisha wakazi mbalimbali, viongozi wa dini, viongozi wa chama na serikali pamoja na wadau wa kijamii, ambapo walipata fursa ya kufuturu kwa pamoja na kuimarisha undugu.
Akizungumza katika tukio hilo, Abdullfatah Priscus Tarimo alisisitiza umuhimu wa kudumisha upendo, kusaidiana na kuendeleza mshikamano wa kijamii bila kujali tofauti za kiimani.
Akitoa neno la shukrani, Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Kilimanjaro, Sheikh Awadhi Lema, alimpongeza Abdullfatah Priscus Tarimo kwa moyo wake wa kujitolea na kuendeleza utaratibu huo kila mwaka, akieleza kuwa ni kitendo chenye baraka kubwa mbele za Mwenyezi Mungu.
Sheikh Lema alisisitiza mafundisho ya dini kwa kunukuu kuwa, “Atakayemfuturisha aliyefunga atapata ujira sawa na wake bila kupunguziwa chochote,” akiongeza kuwa Ramadhani ni kipindi cha kuongeza ibada, kusaidia wenye uhitaji na kuimarisha uhusiano mwema katika jamii.
Alibainisha kuwa jitihada hizo zimekuwa chachu ya kuimarisha umoja na amani miongoni mwa wananchi wa Moshi na maeneo ya jirani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alieleza kufurahishwa na tukio hilo akisema linaimarisha mshikamano na kudumisha amani, huku akihimiza wananchi kuendelea kushirikiana katika shughuli za maendeleo na kuishi kwa kuheshimiana bila kujali tofauti zao.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, alisema kitendo hicho kinaakisi misingi ya kujali watu na kuimarisha ustawi wa jamii, akibainisha kuwa vitendo vya aina hiyo vinapaswa kuungwa mkono na viongozi wengine.
Kwa upande wake, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaaban Mlewa, aliiomba serikali kudhibiti vitendo vya baadhi ya wafanyabiashara kufungua biashara za pombe na kuandaa “disco toto” wakati wa sikukuu ya Eid
Alisema mara nyingi hali hiyo hujitokeza siku ya Idi, jambo ambalo halilingani na maana halisi ya sikukuu hiyo, ambayo ni kumshukuru Mungu baada ya kukamilika kwa ibada ya mfungo wa Ramadhani.
Aliongeza kuwa maombi hayo yamekuwa yakitolewa kila mwaka, akiitaka serikali kuchukua hatua za kuzuia shughuli hizo wakati wa sikukuu, na kuruhusu biashara hizo kuendelea baada ya maadhimisho kukamilika.


















Baraka tele kwake
ReplyDelete