RUWASA KILIMANJARO YAGAWA VITENDEA KAZI KUIMARISHA HUDUMA ZA MAJI VIJIJINI

MOSHI-KILIMANJARO.


WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Kilimanjaro, imegawa vitendea kazi kwa wenyeviti wa vyombo vinavyosimamia utoaji wa huduma za maji ngazi ya jamii (CBWSOs), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za maji vijijini.

Akikabidhi vifaa hivyo katika maadhimisho ya Wiki ya Maji, Meneja wa RUWASA mkoani humo, Mhandisi Weransari Munisi, alisema hatua hiyo inalenga kuimarisha usimamizi, uendeshaji na ukarabati wa miradi ya maji katika maeneo ya vijijini.

Alieleza kuwa vifaa vilivyotolewa ni pamoja na pikipiki sita, spana 80 za kufungia mabomba, vipande 90 vya mabomba (pipeline), vifaa vitatu vya kupima ubora wa maji, misumeno 25 ya kukatia mabomba, misumeno 250 ya kawaida pamoja na chain block 20.

Munisi alisema uwepo wa vitendea kazi hivyo utasaidia viongozi hao kusimamia huduma za maji kwa ufanisi zaidi na kufika kwa wakati katika maeneo yao ya kazi.

Aidha, alibainisha kuwa RUWASA imezingatia ushiriki wa wanawake katika vyombo vya usimamizi wa huduma za maji ngazi ya jamii, akisisitiza kuwa kundi hilo lina mchango mkubwa katika masuala ya maji.

“Wanawake ni kundi ambalo huwezi kulitenganisha na masuala ya maji, kwani wao ndio wahusika wakuu katika utafutaji na matumizi ya maji majumbani,” alisema.

Aliongeza kuwa hapo awali watoto wa kike katika maeneo mengi ya vijijini walikosa fursa ya kupata elimu kutokana na uhaba wa maji, hali iliyowalazimu kutembea umbali mrefu, hadi kilometa 10 kwa siku, kutafuta maji kwa ajili ya familia zao.

Hata hivyo, alisema kwa sasa changamoto hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, jambo lililochangia kuongezeka kwa mahudhurio ya wanafunzi shuleni.

Vilevile, alieleza kuwa upatikanaji wa maji safi umesaidia kupunguza magonjwa ya mlipuko na yale yanayotokana na maji yasiyo salama, kama vile magonjwa ya tumbo na minyoo.

Baadhi ya wenyeviti wa CBWSOs walipongeza Serikali kupitia RUWASA kwa kuwapatia vitendea kazi hivyo, wakisema vitarahisisha utekelezaji wa majukumu yao ikilinganishwa na awali walipokuwa wakitegemea usafiri wa bodaboda.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.