MOSHI-KILIMANJARO.
WANANCHI wametakiwa kuendelea kutunza na kulinda vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali hiyo muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Wito huo umetolewa Alhamisi, Machi 5, 2026 na Afisa Mazingira wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB), Mhandisi Arafa Majid, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Uhuru Park, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhandisi Arafa aliwataka wananchi kuacha tabia ya kutupa taka na kuweka vitu visivyohusika ndani ya mito, akieleza kuwa vitendo hivyo vinachangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa vyanzo vya maji.
Aidha, alisisitiza kuwa shughuli za kibinadamu zinapaswa kufanyika nje ya umbali wa mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji ili kulinda na kuhifadhi rasilimali hiyo muhimu.
Alieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa matumizi mbalimbali ya jamii sasa na katika siku zijazo.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Arafa alitoa elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondari walioshiriki maadhimisho hayo kuhusu umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.
Alibainisha kuwa utoaji wa elimu kwa vijana ni njia mojawapo ya kujenga uelewa wa kudumu kuhusu umuhimu wa kulinda rasilimali za maji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Kiuchumi Manispaa ya Moshi, Joyce Ndossi, aliipongeza Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB) kwa kushiriki katika maadhimisho hayo na kutoa elimu kwa wanafunzi pamoja na wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira.
Alisema ushiriki wa PBWB katika kutoa elimu kwa jamii ya utunzaji wa vyanzo vya maji, unasaidia kuongeza uelewa na kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali za maji kwa manufaa ya jamii ya sasa na vizazi vijavyo.
















