NAIBU WAZIRI MAGHEMBE AANZA ZIARA YA KIKAZI INDIA, KUSHIRIKI MKUTANO WA RAISINA DIALOGUE 2026

 

NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe, ameanza ziara ya kikazi nchini India.

Ambapo pamoja na mambo mengine atashiriki mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje katika jukwaa la Raisina Dialogue 2026 utakaofanyika jijini New Delhi kuanzia Machi 5 hadi Machi 7 mwaka huu.

Katika ziara hiyo, Dkt. Maghembe anamwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.

Mbali na kushiriki mkutano huo wa Kimataifa, Naibu Waziri huyo anatarajiwa kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Dkt. Subrahmanyam Jaishankar, kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na India.

Aidha, akiwa nchini humo atakutana na wawakilishi wa heshima wa Tanzania waliopo India pamoja na kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi nchini humo (Diaspora), ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Serikali na Watanzania walioko nje ya nchi.

Mara baada ya kuwasili nchini India, Dkt. Maghembe alipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Anisa Mbega, katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini New Delhi, Balozi Mbega pamoja na maafisa kutoka Wizara na Ubalozi walitoa taarifa kuhusu maandalizi na ratiba ya ziara hiyo.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.