Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwl. Mwajuma Abbas Nasombe, akiwa mgeni rasmi katika Siku ya Wanawake Duniani, Manispaa ya Moshi iliyofanyika viwanja vya Uhuru Park Machi 5,2026.
MOSHI-KIKIMANJARO.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Moshi imetoa zaidi ya shilingi bilioni 5.9 kama mikopo isiyo na riba kwa vikundi 758 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kipindi cha awamu ya sita ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hayo yalielezwa Alhamisi ya Machi 5,2026 na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Uhuru Park, Manispaa ya Moshi.
Alisema kati ya fedha hizo, vikundi vya wanawake 507 vimenufaika na mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.3, hatua ambayo imeendelea kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za maendeleo.
Aidha, alisema Manispaa ya Moshi imeongezewa fedha za miradi ya maendeleo kutoka shilingi bilioni 38 hadi kufikia shilingi bilioni 56, hatua inayochochea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.
Katika sekta ya elimu, alisema zaidi ya shilingi bilioni 16.6 zimetolewa kusaidia utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo, kuboresha miundombinu ya shule pamoja na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.
Alisema katika sekta ya afya, zaidi ya shilingi bilioni 6 zimetolewa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na dawa muhimu za binadamu katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo aliwataka wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia ipasavyo kwa kuanzisha na kuendeleza miradi yenye tija, pamoja na kuitekeleza kwa weledi ili waweze kurejesha mikopo hiyo kwa wakati kulingana na mikataba waliyoisaini na halmashauri.













