MOSHI-KILIMANJARO.
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Wakili Elizabeth Minde, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ngazi ya mkoa yatakayofanyika Machi 4 mwaka huu katika viwanja vya Kituo cha Afya Bomambuzi, Manispaa ya Moshi mkoani humo.
Akizungumzia maandalizi ya maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Moshi Mjini, Theresia Komba, alisema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Haki kwa Wanawake na Wasichana Msingi wa Maendeleo Jumuishi Dira 2050,” ikilenga kusisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia na haki kama nguzo muhimu ya maendeleo endelevu.
Alieleza kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kutambua na kuenzi mchango wa wanawake katika nyanja za kijamii, kisiasa na kiuchumi, sambamba na kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Komba aliongeza kuwa shughuli mbalimbali za kijamii zilianza kufanyika tangu Machi 1, zikiwemo utoaji wa elimu kwa umma kuhusu Bima ya Afya kwa Wote pamoja na kampeni za uhamasishaji juu ya usawa wa kijinsia.
Alibainisha kuwa kilele cha maadhimisho hayo kimkoa kitafanyika rasmi Machi 4 mwaka huu.
Aidha, aliwataka wananchi na wadau wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho hayo na kuunga mkono jitihada za kulinda na kuimarisha haki za wanawake na wasichana kwa maendeleo ya jamii kwa ujumla.







