MOSHI-KILIMANJARO.
UMOJA wa Wanawake wa Tanzania Wilaya ya Moshi Mjini, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC) na Kilimanjaro Clinical Research Institute (KCRI) chini ya mradi wa NORA, wametoa huduma za bure za uchunguzi na matibabu ya saratani ya matiti na shingo ya kizazi kwa wanawake wa Manispaa ya Moshi.
Hayo yalisemwa jana na Katibu wa UWT Wilaya ya Moshi Mjini, Catherine Sarwatt, wakati wq uzinduI wa maadhimishi ya Siku ya Wanawake Duniani, ambapo kwa wilaya ya Moshi mjini yalifanyika Kata ya Bomambuzi kwenye kituo cha afya Pasua.
"Zaidi ya wanawake 1,000 wamejitokeza kupatiwa huduma hiyo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, ambayo kitaifa inatarajiwa kufanyika Machi 8 Jijini Mwanza."alisema Catherine.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo Mwenyekiti wa UWT Moshi Mjini, Theresia Komba, alisema lengo la zoezi hilo ni kuhamasisha uchunguzi wa mapema na kutoa elimu ya afya ili kupunguza vifo vinavyotokana na saratani hizo.
Alisema saratani ya matiti na shingo ya kizazi imeendelea kuwa tishio kwa maisha ya wanawake wengi, huku wengi wakigundulika wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa.
Kwa upande wake, Daktari Kiongozi wa Kituo cha Afya Pasua, Francis Gwasma, alisema saratani ya mlango wa kizazi huanza taratibu kwa muda mrefu bila kuonyesha dalili, hali inayowafanya wanawake wengi kuchelewa kutafuta matibabu, huku akitoa wito kwa wanawake kujitokeza kupima mara kwa mara ili kulinda afya zao kabla tatizo halijawa kubwa.
Naye Diwani wa Kata ya Bomambuzi, Juma Raibu, alisema Kituo cha Afya Pasua kinakabiliwa na changamoto ya ongezeko la wagonjwa kutokana na kutoa huduma bora zinazovutia wananchi wengi.
Aidha alisema kituo hicho kwa sasa kinahudumia zaidi ya kata saba na kuiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kuongeza bajeti ya vifaa tiba, dawa muhimu na watumishi ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Mmoja wa wananchi waliojitokeza kupima afya, Faiza Mohamed, aliipongeza UWT kwa kuandaa huduma hiyo akisema imewasaidia wanawake wengi kupata uchunguzi kwa wakati bila gharama.












