TAKUKURU KILIMANJARO YAOKOA SH MILIONI 12.2, YABAINI MAPUNGUFU MIRADI 50 YA MAENDELEO

MOSHI-KILIMANJARO.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU mkoani Kilimanjaro imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi milioni 12.2 katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka jana kupitia ufuatiliaji na uchunguzi wa miradi ya maendeleo pamoja na mapato ya Serikali.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa taasisi hiyo, Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo, Musa Chaulo, alisema fedha hizo zimeokolewa baada ya kubaini dosari katika usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma katika maeneo mbalimbali ya mkoa.

Alisema katika uchunguzi uliofanywa Kijiji cha Mwasi Kusini, Kata ya Uru Mashariki, ilibainika kuwa shilingi milioni 2.6 zilizotokana na mauzo ya viwanja hazikuwekwa kwenye akaunti ya kijiji kama ilivyoamuliwa kwenye mkutano wa hadhara.

Katika Wilaya ya Mwanga, TAKUKURU ilibaini matumizi ya vifaa vya ujenzi visivyo na ubora katika miradi ya ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo kwenye baadhi ya shule za msingi.

Wilayani Siha, taasisi hiyo ilibaini kuwa kaya 30 zilizokuwa zikiunganishiwa umeme zilitakiwa kuchangia shilingi 72,000 kila moja kwa madai ya kulipia nguzo za umeme kwa TANESCO, fedha zilizofikia shilingi milioni 2.16, bila kufuata utaratibu rasmi.

Aidha, katika kipindi hicho TAKUKURU ilifuatilia miradi 50 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 21.5 katika sekta za afya, elimu, umeme na barabara, ambapo miradi yote ilibainika kuwa na mapungufu na wahusika kupewa ushauri wa kuyarekebisha.

Kwa upande wa malalamiko, jumla ya malalamiko 96 yalipokelewa, kati ya hayo 55 yalihusu rushwa, ambapo kesi 14 zinaendelea mahakamani, kesi mbili mpya zimefunguliwa na kesi tano zimeamuliwa kwa mafanikio.

TAKUKURU imesema itaendelea kutoa elimu kwa umma na kuimarisha ufuatiliaji wa rasilimali za umma ili kudhibiti vitendo vya rushwa.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.