UWT MOSHI MJINI YASISITIZA MALEZI BORA , ELIMU YA USTAWI WA JAMII, ULIPAJI WA ADA KWA WANACHAMA


MOSHI-KILIMANJARO.


WAZAZI na walezi wameaswa kuimarisha malezi ya watoto pamoja na kutoa mafunzo ya ustawi wa jamii kwa wananchi ili kupunguza changamoto za misongo ya mawazo, migogoro ya kifamilia na matatizo ya kisaikolojia yanayoikumba jamii. 

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Wilaya ya Moshi Mjini, Theresia Komba, wakati wa ziara ya Kamati ya Utekelezaji ya UWT wilayani humo iliyolenga kuhamasisha ulipaji wa ada za uanachama wa jumuiya pamoja na kutoa elimu kuhusu ustawi wa wanawake na malezi bora ya watoto.

Komba amesema kuwa juhudi za kutoa elimu ya ustawi wa jamii zina mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye utulivu, maadili mema na maendeleo endelevu. 

“Niwaombe wazazi na walezi kuendelea kuweka mkazo katika malezi ya watoto wetu sambamba na utoaji wa elimu ya ustawi wa jamii, kwa kuwa 
tunaamini familia imara ndiyo msingi wa jamii imara,” amesema Komba. 

Aidha, amewahimiza wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya familia na jamii huku wakizingatia malezi bora ya watoto ili kujenga taifa lenye maadili mema na kizazi chenye nidhamu.

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo ilitoa elimu kuhusu haki za wanawake, umuhimu wa elimu kwa watoto pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii ikiwemo mmomonyoko wa maadili.

Wanachama na wananchi walioshiriki katika kikao hicho wamepongeza juhudi za viongozi wa UWT Moshi Mjini kwa kuendelea kuwafikia wanawake katika ngazi za chini na kutoa elimu yenye manufaa kwa jamii.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.