HAMPHREY MOSHA; UWANJA WA MAJENGO KUKUZA MAPATO YA MANISPAA YA MOSHI

MOSHI-KILIMANJARO.


DIWANI wa Kata ya Majengo, Humphrey Mosha, amewapongeza madiwani wa Manispaa ya Moshi kwa kuridhia kutengwa kwa kiasi cha Sh bilioni 2.1 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa uwanja wa mpira wa Majengo, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.

Mosha amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya madiwani wa manispaa hiyo kutembelea uwanja huo kwa ajili ya kujionea maendeleo ya ujenzi unaoendelea.

Alisema hapo awali mradi huo ulikwama kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri kuwa madogo, ambapo Manispaa ya Moshi ilikuwa ikikusanya takribani Sh bilioni 6 pekee kwa mwaka, hali iliyosababisha kushindwa kuendeleza ujenzi wa uwanja huo kwa kasi iliyotarajiwa.

Hata hivyo, alisema tangu kuwasili kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, mapato ya ndani yameongezeka kutoka Sh bilioni 6 hadi kufikia Sh bilioni 11, jambo ambalo limewezesha kupatikana kwa fedha za kukamilisha mradi huo mkubwa wa kimichezo.

“Kuongezeka kwa mapato ya ndani kumeiwezesha manispaa kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa uwanja huu, ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na halmashauri kwa ujumla,” alisema Mosha.

Aidha, alisema kukamilika kwa uwanja huo kutatoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa Kata ya Majengo na Manispaa ya Moshi kwa ujumla kupitia biashara zitakazokuwa zikifanyika wakati wa michezo na matukio mbalimbali yatakayokuwa yakifanyika katika eneo hilo.

Aliongeza kuwa uwepo wa uwanja huo pia utaongeza mapato ya ndani ya manispaa kupitia shughuli za michezo na burudani, huku fedha zitakazokusanywa zikielekezwa katika utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo katika kata mbalimbali za manispaa hiyo.

Akizungumza Mhandisi wa Manispaa ya Moshi, Daniel Kileo, amesema kazi zitakazotekelezwa na mkandarasi huyo ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa jukwaa kuu, vyumba vya kubadilishia nguo, vyumba vya waamuzi, eneo la kuchezea mpira, uwekaji wa nyasi bandia zenye viwango vya FIFA, ujenzi wa benchi maalum za timu, uzio wa eneo la kuchezea pamoja na mifumo ya maji safi, maji taka, TEHAMA (ICT) na kamera za usalama.



Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kilimanjaro (KRFA), Abdallah Thabit, ameishukuru Serikali kwa kuridhia utoaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya michezo nchini.

Ujio wa timu mbalimbali za mpira wa miguu kufanya mazoezi Moshi wakati wa mashindano ya AFCON utafungua fursa kubwa ya utalii wa michezo, ambapo wageni hao pia watapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali ikiwemo Mlima Kilimanjaro.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.