TAKUKURU KILIMANJARO YAOKOA MILIONI 16.1




MOSHI-KILIMANJARO


TAASISI  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Kilimanjaro (TAKUKURU) imefanikiwa kusaidia kupatikana kwa fedha za serikali kiasi cha Sh milioni 16.1 katika ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2026.
Hayo yameelezwa jana na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Moshi.


Chaulo alisema TAKUKURU Wilaya ya Hai ilifanya uchunguzi dhidi ya mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ambaye alilipwa mshahara wa Sh milioni 11.4 kuanzia Agosti mwaka 2022 hadi Juni mwaka 2023 bila kuwepo katika kituo chake cha kazi cha Hospitali ya Marangu.

Alisema wakati akilipwa fedha hizo, mtumishi huyo alikuwa akifanya kazi katika Kituo cha Uuguzi Machame kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini.

"Baada ya kubaini hilo, TAKUKURU Wilaya ya Hai ilimtaka mtumishi huyo kurejesha fedha zote ambazo hakustahili kulipwa, ambapo mwezi Machi mwaka huu alirejesha kiasi hicho chote cha Sh milioni 11.4 kupitia akaunti ya NMB PCCB Hai huku hatua nyingine za kisheria zikiendelea".

Aidha, alisema TAKUKURU Kituo Maalumu Holili ilisaidia kusimamisha mkataba usio rasmi kati ya kijiji cha Uparo kilichopo Kata ya Kirua Vunjo na kampuni ya Million Engineering and General Supply Limited, hatua iliyookoa kiasi cha Sh milioni 2.5 za mapato ya kijiji hicho.

Alisema uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU ulibaini kuwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya kijiji hicho na mwekezaji huyo hayakufuata sheria, taratibu na miongozo ya serikali.


Kwa mujibu wa Chaulo, makubaliano hayo yalikuwa yanamtaka mwekezaji kulipa ushuru wa madini ya ujenzi kwa kiwango cha Sh milioni 2 kwa tripu 300 badala ya kiwango halali cha Sh 15,000 kwa kila tripu 30, jambo ambalo lingeisababishia serikali hasara ya mapato.

Katika hatua nyingine, TAKUKURU Wilaya ya Siha ilifanikiwa kuokoa mifuko 63 ya saruji iliyokuwa imenunuliwa zaidi katika mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo katika Shule ya Msingi Olkolili.
Alisema mifuko hiyo ilitumika katika ukarabati wa darasa moja na ofisi moja baada ya kubainika kuwa wahusika walinunua mifuko 105 ya saruji badala ya mifuko 42 iliyokuwa inahitajika.



Sambamba na hilo, TAKUKURU Siha ilisaidia fundi aliyekuwa akitekeleza mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Sabuko kulipwa fedha zake za madai kiasi cha Sh milioni 2.2 ambazo alikuwa hajalipwa licha ya kumaliza kazi kwa muda uliopangwa.

Kwa ujumla, TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro imesema imetoa ushauri wa marekebisho ya mapungufu yaliyojitokeza wakati wa ufuatiliaji wa matumizi ya zaidi ya Sh bilioni 15.2 zilizotengwa kwa utekelezaji wa miradi 46 ya maendeleo katika sekta za afya, elimu na uvuvi mkoani humo.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.