MOSHI-KILIMANJARO.
VIJANA 80 kutoka kata mbalimbali za Jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro wanatarajiwa kupatiwa mafunzo ya ufugaji wa nyuki kwa lengo la kuwawezesha kujitegemea kiuchumi kupitia shughuli za ufugaji wa nyuki.
Hayo yalisemwa Mei 19,2026 na Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Ally Badi, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu maandalizi ya mafunzo hayo yanayotarajiwa kuanza Mei 30 mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.
Badi alisema kila kata kati ya kata 16 za jimbo hilo itatoa vijana watano watakaopata mafunzo ya kina kuhusu ufugaji wa nyuki kwa ajili ya biashara na kuongeza kipato.
Alisema mafunzo hayo yatatolewa na wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, ambapo vijana watajifunza mbinu bora za ufugaji wa nyuki, utunzaji wa mizinga, uvunaji salama wa asali pamoja na njia za kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na nyuki.
Aidha alisema baada ya kuhitimu mafunzo hayo, kila mshiriki atapatiwa mzinga wa kisasa ili kumwezesha kuanza shughuli za ufugaji wa nyuki.
Kwa mujibu wa Badi, programu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa kauli mbiu ya Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Morris Makoi, isemayo “Siasa na Uchumi”, ambapo tayari mbunge huyo ameshatekeleza miradi mingine ya kiuchumi ikiwemo ugawaji wa miche ya kahawa na parachichi.
Pia alisema baada ya mafunzo hayo ya ufugaji wa nyuki, mbunge huyo anatarajia kuendesha mafunzo kwa vijana wanaojihusisha na sekta ya utalii, ambapo zaidi ya vijana 150 watanufaika.
Alisema lengo la programu hizo ni kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea kiuchumi kupitia miradi endelevu inayochangia maendeleo ya familia na jamii kwa ujumla.
Badi aliongeza kuwa ufugaji wa nyuki ni biashara yenye tija kubwa kiuchumi pamoja na mchango wake katika uhifadhi wa mazingira.










