MOSHI-KILIMANJARO.
ZAIDI ya shilingi bilioni 15.9 zimetumika kutekeleza miradi saba ya maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambayo itatembelewa na Mwenge wa Uhuru Julai 2 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru.
Amesema miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa Barabara ya Makanya katika Kata ya Majengo uliogharimu shilingi milioni 295, ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Lucy Lameck kwa gharama ya shilingi milioni 50, pamoja na ujenzi wa jiko la kisasa linalotumia nishati safi lililogharimu shilingi milioni 30.
Aidha, amesema Mwenge wa Uhuru utatembelea mradi wa chanzo cha maji cha Moshi uliogharimu shilingi milioni 646, utakaoboreshwa huduma ya maji kwa wananchi, pamoja na kuzindua Kituo cha Polisi cha Kata ya Karanga kilichojengwa kwa nguvu za wananchi kwa gharama ya shilingi milioni 119.
Mnzava amesema pia Mwenge wa Uhuru utatembelea kikundi cha vijana cha B5 Media kilichopo Kahawa House, ambacho kilinufaika na mkopo usio na riba wa shilingi milioni 45.5 kupitia mpango wa uwezeshaji wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Ameongeza kuwa Mwenge wa Uhuru utatembelea ukumbi mkubwa wa mikutano uliojengwa na Kampuni ya Mahina Holding kwa gharama ya shilingi bilioni 4.7, pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC, ambapo utazindua mradi wa ujenzi wa vyumba nane vya upasuaji uliogharimu shilingi bilioni 9.9.
Kwa mujibu wa Mnzava, kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 ni "Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo," ikilenga kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Mbali na ujumbe huo, Mwenge wa Uhuru utaendelea kuhamasisha mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, malaria, matumizi ya dawa za kulevya na rushwa, pamoja na kuhimiza lishe bora ili kukabiliana na tatizo la utapiamlo.


