ZUBERI CUP-2026 KUANZA KUTIMUA VUMBI JULAI 11,2026, TIMU 36 KUSHIRIKI

MOSHI-KILIMANJARO.

MASHINDANO ya soka ya Zuberi Cup 2026 yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai 11 mwaka huu katika Viwanja vya Reli Njoro, huku jumla ya timu 36 zikitarajiwa kushiriki katika michuano hiyo inayolenga kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana.

Akizungumza na Kisena Blogs leo Juni 25, 2026, Mratibu wa mashindano hayo, Mwalimu Japhet Mpande, amesema maandalizi ya kuelekea mashindano hayo yanaendelea vizuri na kwamba msimu huu utakuwa mkubwa zaidi kuliko misimu iliyopita.

Amesema uzinduzi rasmi wa msimu wa sita wa Zuberi Cup utafanyika Julai 4, 2026 katika Viwanja vya Hugos, ambapo timu zote zitashiriki katika shughuli mbalimbali za maandalizi kabla ya kuanza kwa michuano hiyo.

Mpande amesema waandaaji wamejipanga kuhakikisha mashindano yanaendeshwa kwa kiwango cha juu ili kuongeza ushindani na kuvutia mashabiki wengi wa soka.

“Tunatarajia msimu huu uwe bora zaidi kuliko uliopita kwa upande wa maandalizi, usimamizi na ushindani wa timu zitakazoshiriki,” amesema Mpande.

Ameeleza kuwa Zuberi Cup imeendelea kukua na kupata umaarufu mkubwa tangu ilipoanzishwa, huku ikitoa fursa kwa vijana wengi kuonesha vipaji vyao na kupata nafasi ya kuonekana na wadau mbalimbali wa soka.

Huu ni msimu wa sita wa mashindano hayo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021, ambapo katika msimu uliopita wa mwaka 2025 timu ya Afro Boys iliibuka bingwa baada ya kufanya vizuri katika hatua mbalimbali za mashindano.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ongezeko la idadi ya timu na maandalizi yaliyofanywa na waandaaji kuelekea msimu wa mwaka huu.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.