RAIS SAMIA SULUHU HASSAN, KUZINDUA JENGO LA SARATANI KCMC JUNI 24,2026

MOSHI-KILIMANJARO.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa jengo la huduma za wagonjwa wa saratani lililojengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC, mkoani Kilimanjaro.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alipokuwa akizungumza na wananchi mara baada ya kushiriki matembezi ya amani yaliyofanyika mjini Moshi mwishoni mwa wiki, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru unaotarajiwa kuwasili wilayani humo mwishoni mwa mwezi huu.

Mnzava alisema Rais Samia anatarajiwa kuwasili mkoani Kilimanjaro Juni 24, mwaka huu, ambapo atakwenda moja kwa moja katika Hospitali ya KCMC kwa ajili ya kushiriki hafla hiyo muhimu ya uzinduzi.

Alisema kabla ya uzinduzi rasmi, Rais atapata fursa ya kutembelea jengo hilo na kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, ambao unatarajiwa kuboresha huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani kwa wananchi wa Kanda ya Kaskazini na maeneo mengine ya nchi.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais pamoja na kushiriki katika hafla hiyo itakayofanyika katika viwanja vya Hospitali ya KCMC.

Kuhusu ujio wa Mwenge wa Uhuru, Mnzava alisema unatarajiwa kuingia Manispaa ya Moshi mwezi Julai mwaka huu, ambapo utakagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali na wananchi.

Alisema Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa kuhamasisha uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi, hivyo amewahimiza wakazi wa Moshi kujitokeza kwa wingi kushiriki shughuli zote zitakazoambatana na mbio hizo.

“Wananchi watapata fursa ya kujionea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao wakati Mwenge wa Uhuru utakapokuwa ukikagua, kuweka mawe ya msingi au kuzindua miradi hiyo,” alisema Mnzava.

Aliongeza kuwa ujio wa Rais Samia pamoja na Mwenge wa Uhuru ni matukio muhimu yatakayotoa fursa ya kuonesha mafanikio ya maendeleo yaliyopatikana katika Mkoa wa Kilimanjaro kupitia uwekezaji wa Serikali katika sekta mbalimbali za huduma za jamii.










F



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.