VIWANJA VINNE KUTUMIKA MASHINDANO YA ZUBERI CUP-2026


Uwanja wa Mandela  ulioko Kata ya Bomambuzi,  ni miongoni mwa viwanja vinne ambavyo vitatumika  katika mashindano ya Zuberi Cup-Tournament 

MOSHI-KILIMANJARO.


MAANDALIZI ya Mashindano ya Zuberi Cup-2026 yanazidi kushika kasi huku viwanja vinne vilivyoteuliwa kutumika katika mashindano hayo vikiendelea kufanyiwa maboresho ya mwisho tayari kwa michuano inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Julai 11 mwaka huu.

Mratibu wa mashindano hayo, Mwalimu Japhet Mpande, ameyasema hayo wakati akizungumza na Kisena Blogs, kuhusiana na marekebisho ya uwanja wa Mandela.

Mpande amesema uwanja wa Mandela tayari wameanza kufunga mabenchi kwa ajili ya waamuzi na viongozi wa timu, huku kazi ya kuweka alama za vipimo vya uwanja, maeneo ya magoli, benchi za waamuzi, viongozi pamoja na sehemu za mashabiki ikiendelea.

"Tupo hapa leo kuhakikisha vipimo vyote vya uwanja vinawekwa kwa usahihi ili kukidhi matakwa ya mashindano na kuhakikisha timu pamoja na mashabiki wanapata mazingira bora ya mchezo," alisema Mpande.

Aidha amevitaja viwanja vitakavyotumika katika mashindano hayo ni pamoja na Uwanja wa Mandela uliopo kata ya Pasua, uwanja wa Railway uliopo Kata ya Njoro, Uwanja wa KDC uliopo Kata ya Kiboriloni na Uwanja wa Memorial uliopo Kata ya Soweto.

Amesema maboresho ya viwanja hivyo yanaendelea vizuri, huku Uwanja wa Mandela ukiwa tayari umekamilika kwa kiasi kikubwa baada ya kupandwa nyasi na kufanyiwa matengenezo mbalimbali ili kukidhi viwango vya mashindano.

"Kwa sasa kinachoendelea katika uwanja wa Mandela ni marekebisho madogo, ikiwemo kung'oa magugu yasiyotakiwa pamoja na kukamilisha maandalizi mengine ya mwisho.'amesema Mwl. Mpande.

Aidha, amesema katika uwanja wa KDC tayari magoli yamefungwa, wakati uwanja wa Memorial unaendelea kusafishwa ili kuuweka katika hali nzuri ya kutumika, na kwamba ifikapo Julai 11 viwanja vyote vitakuwa tayari kupokea mechi za mashindano hayo.

Kwa upande wake, muandaaji wa mashindano hayo, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya uwanja wa Mandela na kueleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika maboresho yake.

Baada ya hapo, Kidumo alitembelea pia uwanja wa Railway uliopo Kata ya Njoro, ambako alipokea taarifa ya maendeleo ya maandalizi na kuwataka wasimamizi wa viwanja hivyo, kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati ili mashindano yaanze katika mazingira bora.

Amesema lengo la mashindano ya Zuberi Cup-2026 si kuibua vipaji vya wachezaji pekee, bali pia kuacha urithi wa kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo katika Manispaa ya Moshi, hatua itakayowanufaisha wanamichezo na jamii kwa ujumla hata baada ya mashindano kumalizika.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.