VILABU VYAMPONGEZA MSTAHIKI MEYA ZUBERI KIDUMO UBORESHAJI WA UWANJA WA MANDERA , VYATAMBA KUJIPANGA ZUBERI CUP-2026

MOSHI-KILIMANJARO.


VLABU vinavyotarajia kushiriki mashindano ya Zuberi Cup-2026 vimepongeza hatua ya kuendelea kuboreshwa kwa miundombinu ya Uwanja wa Soka wa Mandela uliopo Kata ya Bomambuzi, vikisema hatua hiyo itaongeza ubora wa mashindano na kuchochea maendeleo ya soka kwa vijana.

Kocha wa timu ya Mandela Sports Centre, Azidu Iddi Kiojo, amesema uboreshaji wa uwanja huo ni jambo la kujivunia na utatoa mazingira salama na bora kwa wachezaji, hususan vijana wanaokuza vipaji vyao.

Alimshukuru Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, kwa juhudi za kuboresha viwanja vya michezo, akieleza kuwa hapo awali mazingira ya uwanja huo hayakuwa rafiki kwa mazoezi na mashindano.

"Kukamilika kwa uwanja huu hakutawanufaisha washiriki wa Zuberi Cup pekee, bali pia kutavutia timu mbalimbali kuja kufanya mazoezi na mashindano hapa Moshi," alisema Kiojo.

Kuhusu maandalizi ya mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Julai 11 mwaka huu, Kiojo alisema timu yake imejipanga kikamilifu kufanya vizuri, akibainisha kuwa Zuberi Cup imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza vipaji vya wachezaji wengi ambao sasa wanacheza Ligi Kuu Tanzania Bara na wengine katika ligi za nje ya nchi.

Aidha, aliwataka washiriki wote wa mashindano hayo kuheshimu sheria za mchezo na kukubali matokeo yanayotokana na ushindani wa uwanjani.

"Soka ni mchezo wa ushindani wenye matokeo ya aina mbalimbali. Ni muhimu kila timu ikakubali matokeo ili kuepusha vurugu ambazo zinaweza kuharibu taswira nzuri ya mashindano haya," alisema.


Kwa upande wake, Mratibu wa Mashindano ya Zuberi Cup, Mwalimu Japhet Mpande, alisema uboreshaji wa Uwanja wa Mandela unaonyesha dhamira ya Mstahiki Meya Zuberi Abdallah Kidumo ya kuwekeza katika maendeleo ya michezo na kuboresha mazingira ya vijana na jamii kwa ujumla.

Alisema pamoja na kuboresha viwanja, kazi zinazofanyika zitayafanya mazingira ya Manispaa ya Moshi kuwa ya kuvutia zaidi kwa shughuli za michezo na matukio mengine ya kijamii.

Mpande alisema matarajio ni kwamba ifikapo Julai 11, mwaka huu, viwanja vyote vitakuwa vimekamilika na tayari kwa kutumika wakati wa kuanza kwa mashindano hayo.

Aliongeza kuwa uwekezaji huo utasaidia kufikia viwango bora vya uendeshaji wa mashindano, kuvutia matukio makubwa ya michezo na kufungua fursa kwa vijana kujiajiri na kujenga taaluma kupitia michezo.

Pia aliwataka wakazi wa eneo la Pasua na maeneo jirani kushiriki katika kulinda na kutunza miundombinu ya uwanja huo ili uweze kudumu na kuendelea kunufaisha jamii kwa muda mrefu.

Alisisitiza kuwa utunzaji wa miundombinu ya michezo ni jukumu la kila mwananchi na akampongeza Meya Zuberi Kidumo kwa mchango wake katika kuinua sekta ya michezo ndani ya Manispaa ya Moshi.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.