ZUBERI CUP-2026 KUZIKUTANISHA TIMU 36 MOSHI

MOSHI-KILIMANJARO.

TIMU 36 zinatarajiwa kushiriki mashindano ya soka ya Zuberi Cup-2026 yatakayoanza rasmi Julai 11 mwaka huu katika viwanja vya Njoro, huku waandaaji wakiahidi ushindani mkubwa na maandalizi bora kwa timu zote zitakazoshiriki.
Akizungumza Juni 22,2026 na waandishi wa habari mjini Moshi, Mwenyekiti wa Mashindano hayo, Mwl. Japhet Mpande, alisema uzinduzi rasmi wa msimu wa sita wa Zuberi Cup utafanyika Julai 4, 2026 katika viwanja vya Kili Home, ambapo timu zote zitashiriki katika shughuli mbalimbali za maandalizi ya mashindano.

Mpande alisema tayari waandaaji wamekutana na viongozi wa vilabu vyote vinavyoshiriki kwa ajili ya kupokea na kukagua fomu za usajili wa wachezaji ili kuhakikisha hakuna mchezaji aliyesajiliwa katika zaidi ya timu moja, hatua inayolenga kudumisha haki na ushindani wa mashindano hayo.

Alieleza kuwa katika hafla ya uzinduzi, kila timu itakabidhiwa mipira miwili, nakala za kanuni za mashindano pamoja na ratiba rasmi ya michezo itakayochezwa katika kipindi chote cha mashindano.

Aidha, alisema uzinduzi huo utafuatiwa na upigaji kura wa mechi ya ufunguzi utakaobainisha timu mbili zitakazoshuka dimbani katika mchezo wa kwanza wa mashindano hayo Julai 11 kwenye viwanja vya Njoro.

Kwa mujibu wa Mpande, Zuberi Cup ilianzishwa mwaka 2021 na imeendelea kukua kwa kasi kutokana na kuvutia timu nyingi zaidi kila mwaka, jambo ambalo limeongeza ushindani na kuibua vipaji vya vijana katika mchezo wa soka.

Alibainisha kuwa katika msimu wa mwaka 2025 zaidi ya timu 46 zilishiriki mashindano hayo, huku timu ya Afro Boys ikitwaa ubingwa baada ya kuifunga Msaranga FC katika mchezo wa fainali.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuvutia mamia ya mashabiki wa soka kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro na mikoa jirani, huku yakitajwa kuwa miongoni mwa mashindano makubwa ya ngazi ya jamii yanayochangia maendeleo ya soka la vijana nchini.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.